Inspekta Mkuu wa polisi Douglas Kanja amesema kuna tofauti ya matukio yaliyofuatia madai ya utekeji wa Mbunge wa Juja George Koimbori.
Katika kikao na wanahabari Jumanne, Kanja amesema eneo linaloonekana katika video iliyosambaa mitandaoni ikionesha mahali ambapo Koimbori anadaiwa kutupwa ni tofauti kabisa na eneo lenyewe.
Kulingana na Kanja maafisa wa DCI walilitembelea eneo hilo ambapo ni kwenye shamba la kahawa ili kubaini ukweli. Hata hivyo baada ya ukaguzi wa kina walibainisha kuwa eneo hilo ni tofauti na lile kwenye video ya Koimbori iliyosambazwa mitandaobi.
Aidha maafisa hao walienda katika Hospitali ya Plainsview ambako Koimbori alipelekwa mara ya kwanza ila madaktari hawakutoa taarifa kuhusu huduma za matibabu alizopewa..
Tayari watu watano wamehojiwa kufuatia tukio hilo. Kanja amesema uchunguzi zaidi unaendelea na wote waliohusika watachukuliwa hatua kali.
Ikumbukwe Koimbori amekuwa akichunguzwa kufuatia madai ya ulaghai wa ardhi na tayari Idara ya Upelelezi DPP ilikuwa imetoa agizo la kushtakiwa kwa mbunge huyo.
Ijumaa mbunge huyo alidai kuwa alifanikiwa kutoroka kutoka kwa watu aliowataja kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wanataka kumkamata.
Aidha polisi wamesema Jumatatu usiku maafisa walitumwa kuendeleza uchunguzi na kumhoji mbunge huyo katika Hospitali ya Karen ila hawakuruhusiwa kumwona wakiarifiwa kuwa ni familia tu ndiyo ingepewa idhini ya kumwona.
Mapema Jumanne viongozi wa upinzani wamemembelea Koimbori hospitalini huku wakidai kuwa utekaji nyara dhidi yake umetekelezwa na serikali.
Viongozi hao Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Justin Muturi na Mithika Linturi wamesema watahakikisha haki inapatikana kwa mbunge huyo.
Koimbori alidaiwa kutekwa nyara Jumapili alipokuwa akitoka kanisani kisha akapatikana Jumatatu asubuhi katika shamba la kahawa katika eneo la Githunguri.