Rais William Ruto anaongoza Hafla ya Kitaifa ya Maombi katika Hoteli ya Safari Park jijini Nairobi.
Viongozi wakuu serikalini na wabunge wanahudhuria hafla hiyo ambayo pia imeambatana na Kiamsha kinywa. Zaidi ya wageni elfu tatu pia wanahudhuria kuhudhuria.
Waandalizi wanasisitiza kwamba ni fursa ya kutafakari na kuhubiri upendo na umoja wa taifa
Wazo la Maombi ya Kitaifa lilianzishwa na Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka mwaka wa 1987 alipoalikwa Marekani wakati huo akiwa Naibu wa Spika wa Bunge la Kitaifa na Waziri Msaidizi kuhudhuria hafla ya maombi ya kitaifa.
Mwaka wa 1988 Spika wa Bunge Moses Keino wakati huo alifurahishwa na wazo hilo la Kalonzo na wenzake waliohudhuria hafla ya maombi marekani kwamba wabunge wa Kenya waige.
Mwaka wa 1990 hafla hiyo iliandaliwa nchini na kuongozwa na Rais Daniel Arap Moi. Hata hivyo, kutokana na matukio ya kisiasa wakati huo ambapo serikali ya Moi ililaumiwa na wengi kwa uongozi wa kiimla, hafla hiyo haikufanyika tena hadi mwaka wa 2003 baada ya uchaguzi mkuu ambapo mbunge David Musila alianzisha makundi ya maombi yaliyowashirikisha vigogo wa siasa bungeni akiwemo Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Uhuru Kenyatta wakati huo akiwa kiongozi wa upinzani.
Tangu mwaka huo hafla hiyo imeandaliwa kila Alhamisi ya mwisho ya mwezi Mei hadi mwaka huu ambapo imerejeshwa nyuma hadi Jumatano.
Written by Collins Lusweti