Mamia ya maelfu ya watu wanaougua saratani ya kichwa na shingo iliyoendelea sasa wanaweza kuishi kwa muda mrefu bila saratani hiyo kurudi. Hatua hii ni baada ya kubainika kuwa dawa ya kinga ya jaribio la kimatibabu imefanikiwa kuimaliza saratani aina hiyo kwa kiwango kikubwa na hata kuwawezesha waathiriwa kuendelea kuishi kwa muda mrefu.

Kulingana na wanasayansi na watafiti hiyo ni ishara ya kwanza ya mafanikio kwa wagonjwa walio na saratani hiyo ambayo imekuwa ngumu kutibu kwa miaka 20 sasa.

Dawa ya kinga ya pembrolizumab inaweza kudhibiti saratani ya kichwa na shingo kwa muda mrefu mara mbili ikilinganishwa na matibabu ya kawaida.

Pembrolizumab huweka kinga ya mwili kuikabili saratani kwa kulenga protini maalum ambayo huwezesha dawa hiyo kuangamiza seli za saratani.

Kwa mujibu wa jaribio la kimatibabu baadhi ya wagonjwa, dawa hiyo iliizuia saratani kurudi kwa wastani wa miaka mitano, ikilinganishwa na miezi 30 pale ilipoongezwa kwenye matibabu ya kawaida.

Matokeo hayo yaliwasilishwa kwenye mkutano wa kila mwaka wa Muungano wa Wataalam wa Matibabu ya Saratani (American Society of Clinical Oncology), ambao ni mkutano mkubwa zaidi duniani kuhusu saratani.

Jaribio hilo, lililowahusisha zaidi ya wagonjwa 700 katika vituo 192 katika nchi 24, liliongozwa na watafiti kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Washington.

Watafiti kutoka kote duniani walijaribu dawa hiyo kwa wagonjwa waliogunduliwa hivi karibuni na saratani ya kichwa na shingo iliyoenea lakini bado iko katika hatua ya mwanzo. Mamia ya maelfu ya wagonjwa hugunduliwa na saratani hizi kila mwaka kote duniani.

Miongoni mwa wagonjwa 714 waliokuwa kwenye jaribio hilo, 363 walipokea pembrolizumab wakifuatiwa na matibabu ya kawaida, huku 351 wakipokea tu matibabu ya kawaida upasuaji wa kuondoa uvimbe ukifuatiwa na mionzi (radiation), ikiwa na au bila chemotherapy.

Matibabu ya kawaida hayajabadilika kwa zaidi ya miaka 20 kwa aina hiyo ya wagonjwa, na zaidi ya nusu yao huwa hawaishi zaidi ya miaka mitano baada ya kugunduliwa.

Immunotherapy ilifanya kazi vizuri hasa kwa wagonjwa waliokuwa na viwango vya juu vya alama ya kinga ya mwili inayojulikana kama PD-L1, lakini pia iliongeza kwa kiwango kikubwa uwezekano wa wagonjwa wote wa saratani ya kichwa na shingo kubaki katika hali nzuri bila ugonjwa kuendelea au kurudi.

Saratani kichwani na shingoni ni ngumu kutibu na kumekuwa na mabadiliko kidogo katika jinsi wagonjwa wanavyotibiwa katika miongo miwili.