Shirika la Kenya Association for the Welfare of people With Epilepsy ‘KAWE’ linalojihusisha na masuala na masilahi ya wanaougua kifafa nchini liko katikaTaita Taveta katika juhudi za kuelimisha wahudumu wa afya na jamii kwa jumla jinsi ya kukabili ugonjwa wa kifafa.

Shirika hilo liliandaa hafla ya kuwahamasisha wahudumu wa afya katika Hosipitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi ambapo walielimishwa kuhusu ujuzi wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa kifafa.

Kulingana na Patric Ngechu, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo ni kuwa lengo lao nikuhamasisha umma na wahudumu wa afya ili kuangamiza unyanyapaa na kukabili changamoto za kifafa.

“Tunakadiria asilimia mbili ya wananchi wa Kenya wanaishi na ugonjwa wa Kifafa, ambayo ni kama watu Milioni moja hivi. Changamoto ambayo tunaishuhudia kote nchini ni Ufahamu, Matibabu na Unyanyapaa ndiposa tuko hapa Taita Taveta kushirikiana na Serikali ya kaunti hii katika kukabili changamoto hizi. Hofu yetu kuu ni suala la Matibabu ambapo wengi ya watu hawa wa kifafa hawapati huduma wanazostahili.” Ngwchu alisema.

Kauli yake Ngechu ilisisitizwa na wahudumu hao wa afya ambao walidai wengi wanakosa kujitokeza kwa matibabu na badala yake kutafuta mbinu tofauti za usaidizi.

“Kifafa imekua ndonda ndugu sana katika jamii sababu watu wengi wamajificha na wanaona hao wagonjwa ni kama waliojazwa na mapepo, badala yakuwapeleka Hosipitali, wanawapeleka kwa Maombi na kwa Waganga.” Alisimulia mhudumu wa afya.

Hata hivyo, wito umetolewa kwa jamii kuwakumbatia watu wanaoishi na ugonjwa wa kifafa, vilevile kutakiwa kuwasajili katika shirika la watu wenye ulemavu.

Fatuma Kadzo ambaye ni afisa wa walemavu kaunti ya Taita Taveta amesema Kifafa ni ugonjwa ulioorodheshwa kama moja wapo ya aina ya Ulemavu.

“Kifafa ni ugonjwa unaoharibu ubongo, na kutokana na asilimia ya uharibifu mtu huyo anawekana kupata hali ya matatizo ya ulemavu wa kiakili, na wale wanaopata matibabu na kutumia vyema dawa zao huishi maisha ya kawaida, na wale ambao huzidiwa mara nyingi jamii ndio huwa imewatelekeza.” Alieleza Kadzo

Kulingana Mkurugenzi wa shirika hili la ‘KAWE’ ni kwamba kufikia sasa limezuru kaunti kumi na nane, hii ya Taita Taveta ikiwa kaunti ya kumi na tisa wakilenga kuzuru kaunti zote arobaini na saba nchini Kenya.

Written by Julius Mariki