Maandamano yanafanyika katika miji mbalimbali nchini huku wanaharakati wakilalamikia mauaji ya mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang’, aliyefariki akiwa katika seli za polisi.
Maandamano yanafanyika jijini Nairobi, Mombasa, Kilifi na maeneo mengine huku polisi wakiimarisha doria.
Jijini Nairobi makabiliano yamezuka baina ya polisi na makundi mawili ya waandamanaji huku polisi wailazimika kutumia vitoza machozi kuwatawanya.
Kundi moja linaaminika kuwa la wanaharakati wanaoshinikiza haki kwa familia ya Ojwang’ na jingine likisemekana kuchochewa na baadhi ya viongozi wa kaunti ya Nairobi wanaopinga maandamano.
Mapema Jumanne kundi la wanaume waliokuwa kwenye pikipiki waliwasili katikati ya Jiji la Nairobi huku likidaiwa lilikuwa limepanga kuingilia maandaamano ya amani.
Baadhi ya waliokuwa miongoni mwa kundi hilo walivamiwa huku pikipiki zao zikiteketezwa kwa kuhusishwa na wahuni waliokuwa wamekuja kuyasambaratisha maandamano hayo.
Aidha mwanaharakati Hanifa Hassan ambaye yuko katika mstari wa mbele kupaga maandamano hayo amedai kushambuliwa na watu aliowatambua kuwa maafisa wa polisi wakati wa maandamano hayo.
Jijini Mombasa wanaharakati watatu wanaendelea kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central baada ya kukamatwa mapema Jumanne kwa kuongoza maandamano bila kibali kutoka kwa polisi.
Maandamano hayo ambayo pia yamefanikishwa na kampeni kupitia mitandao ya kijamii hasa ule wa X chini ya alama ya reli #MaandamanoTuesday, yamefanyika licha ya Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Eliud Lagat, kujiondoa kwa muda kupisha uchunguzi.

Lagat amehusishwa na mauaji ya Ojwnag’ hasa ikizingatiwa ndiye aliyekuwa mlalamishi mkuu na kusababisha akamatwe.
Wanaharakati wanashinikiza Lagat kujiuzulu kabisa wadhfa wake wakisema hafai kuendelea kushikilia nafasi hiyo.