Wanawake katika Eneo Bunge la Wundanyi kwenye Kaunti ya Taita Taveta wameandamana hadi kwa ofisi ya Naibu Kamishina kulalamikia kisa cha hivi majuzi ambapo mtoto wa miaka sita alidhulumiwa na kuuliwa kisha mwili wake kutupwa katika kidimbwi cha maji ya kuwafuga Samaki eneo la Kese, lokesheni ya Werugha.

Wakiwa wamebeba mabango ya jumbe mbalimbali za kudai haki na kukomesha dhulma za kijinsia na kuwadhulumu Watoto, wanawake hao wakiongozwa na Kundi la Saunti ya Wanawake wamelishtumu vikali tukio hilo la kuuliwa kwa msichana wa gredi ya pili, lililotokea tarehe 18 mwezi huu wa juni mwaka 2025.

“Kama jamii tumepigwa na mshtuko kutokana na tulio la tarehe 18/6/2025 na kuingiwa na hofu kuhusu Watoto wet una wanafunzi katika kaunti hii kutokana na ongezeko la visa hivi. Tunaitaka idara ya usalama na taasisi zote za serikali kuchukua hatua za dharura kukomesha visa hivi” alieleza msemaji wao.

Wanawake hao wametoa wito kwa Idara ya Usalama na serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mshukiwa wa ukatili huo ili kuwa funzo kwa wengine wote wenye tabia kama hiyo.

Vilevile wamewalaumu baadhi ya watu ambao wanaendelea kuficha maovu haya yanapotendeka katika jamii kutokana na hali kwamba ni watu wa familia ama ukoo mmoja.

“Jamani tukiona visa kama hivi tusinyamaze…wanaodhulumu wako miongoni mwetu, na wengine wetu sisi tunawajua, hivyo tunaomba idara ya usalama iharakishe na mtoto huyu apate haki.” Alisema Mary Mwangola.

Naibu Kamishina wa eneo la Wundanyi Jane Kaitati, katika kuwapokea waandamanaji hao nje ya ofisi yake, amesema kwamba tayari mshukiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea akiwahakikishia kwamba hatua za kisheria zitafuatwa kikamilifu na haki kwa mtoto huyo kupatikana.

“Kama mkuu wa Usalama Wilaya ya Taita, ninawahakikishia kwamba, mshukiwa ameshashikwa, ametiwa mbaroni na atafikishwa mahakamani na tuna Imani na kuomba kwamba haki kwa mtoto wetu itafanyika.” Alisema Jane, naibu kamishina.

Mtoto huyo aidha anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatano tarehe 25 Juni mwaka 2025 katika Kijiji cha Kese Werugha kwenye Eneo Bunge la Wundanyi.

Written by Julius Mariki