Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Abdulhalim Hussein, amefariki Dunia akiwa nyumbani kwake Tudor, Mombasa usiku wa kuamkia Alhamisi.
Ataswaliwa katika Masjid Nuru katika eneo la Bondeni leo alasiri, na kuzikwa katika maziara ya Kikowani.
Viongozi wa dini ya Kiislamu wameendelea kumuomboleza kadhi mkuu, kama aliyekuwa kiongozi imara wa maswala ya sheria ya dini hiyo.
Imam wa msikiti wa Jamia jijini Nairobi, ameandika katika kurasa zake za kijamii. “Indeed we belong to Allah, and indeed, to him we return”
Sheikh Abu Qatada, kiongozi wa dini katika Kaunti ya Mombasa naye ameandika, ”Ee mwenyezi mungu msamehe na umrehemu, na umuigize katika pepo ya juu kabisa.”
Kazi ya Kadhi Mkuu wa Kenya imetambulika kikatiba katika ibara ya 170, kuongoza mahakama ya kadhi kwa ajili ya kushugulikia masuala ya sheria ya kiislamu.
Majukumu ya Kadhi Mkuu ni pamoja na kusikiliza na kuamua kesi za ndoa, talaka, urithi na masuala mengine ya kifamilia kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Ofisi yake, ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali kuhusu masuala ya sheria ya Kiislamu, yanayohitaji maamuzi ya kisheria. Pia, alitoa muongozo kuhusu tarehe za sikukuu muhimu kwa Waislamu nchini Kenya, kama vile tarehe za kuanza na kumalizika kwa mfungo wa Ramadan, baada ya kuonekana kwa mwezi.
Viongozi wa kisiasa wamemwomboleza Kadhi Abdulhalim Hussein. Waziri wa Afya Aden Duale, amemwomboleza kadhi mkuu kama aliyekuwa msomi mkubwa na kiongozi mnyenyekevu.
Ameandika katika ukurasa wa X, “Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe na umrehemu, mpe nguvu na umsamehe. Uwe mkarimu kwake, na umpanulie mlango wa kuingia peponi.
Ewe Mwenyezi Mungu, linda familia yake na uwape subira wakati huu wa maombolezo.”
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, naye amesikitishwa na kifo cha kadhi mkuu. Ameandika,
”Nimesikitishwa mno na kifo cha Kadhi mkuu wa Kenya, Sheikh Abdulhalim Hussein. Hakika sisi ni wa Allah na hakika kwake tutarejea. Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, aliitumikia Ummah wa Kenya kwa kujitolea katika njia nyingi.
Mwenyezi Mungu amsamehe, amuongezee thawabu kwa mema aliyoyatenda, na amkirimie daraja za juu kabisa katika Pepo. Ameen.”
Sheikh Abdulhalim Hussein, aliteuliwa kuwa Kadhi mkuu wa Kenya na tume ya huduma za mahakama (JSC) tarehe 17 Julai 2023, akichukua nafasi ya Sheikh Ahmed Muhdhar, ambaye alistaafu baada ya kuhudumu kwa miaka 12 alipofikia umri wa lazima wa kustaafu wa miaka 60.
Written by Paul Muniu