Katika hatua ya kihistoria ya kuinua maisha ya wavuvi wa Ziwa Victoria, Serikali ya Kaunti ya Kisumu imekamilisha ujenzi wa boti tano za kisasa za uvuvi na boti moja ya doria,juhudi muhimu zinazolenga kuboresha usalama, ufanisi, na heshima ya wavuvi katika fukwe tano za kaunti.
Gavana wa Kisumu, Prof. Anyang’ Nyong’o, alitangaza mafanikio haya wakati wa ziara ya heshima kutoka kwa Edward Omol wa Kenya Shipyards Limited na Afisa Mkuu Mtendaji wa Lakefront Development Corporation, Paul Njanja, katika afisi yake yake ya City Hall. Gavana alieleza kuwa watu wengi wamefariki dunia kutokana na matumizi ya boti hafifu zilizotengenezwa kwa mbao laini.
“Hatua hii ni muhimu sana katika kuzuia vifo hivi vya kusikitisha na kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata riziki bila kuhatarisha maisha yao,” alisema Prof. Nyong’o.
Kila boti ya uvuvi imeundwa kwa ustadi mkubwa na ina injini zenye nguvu kati ya 25 hadi 40 horsepower. Pia, zimewekewa masanduku ya baridi (cooler boxes) yenye uwezo wa kuhifadhi hadi kilo 500 za samaki, hii ikilenga kuhakikisha samaki wanabaki safi hadi sokoni.
Kwa kuimarisha usalama wa wavuvi, kila boti imeambatana na vifaa muhimu vya usalama; vikiwamo
Mavazi ya kujiokoa (life jackets)
Flares kwa dharura na
Vifaa vya usalama vya ziwani
Boti hizo tano zitagawiwa kwa wavuvi katika kaunti ndogo tano ikiwa ni, Seme kwenye kituo cha samaki cha Wanga, Kisumu ya Magharibi kwenye kituo cha Samaki cha Rota, Nyakach kwenye kituo cha Samaki cha Koguta, na Kadibo kwenye kituo cha samaki cha Nyamware.

boti ya sita, ambayo ni ya doria, itakabidhiwa kwa Idara ya Uvuvi kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za uvuvi katika ziwa.
Kwa mujibu wa uongozi wa Kisumu, mradi huu si wa miundombinu pekee, ni ujumbe wa matumaini. Ni uthibitisho wa dhamira ya Kisumu kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia salama, endelevu, na yenye kuwaheshimu wavuvi kama nguzo muhimu ya usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.
Kadri mawimbi ya Ziwa Victoria yanavyogonga fukwe za Kichinjio, Wanga, Rota, Kogura, na Nyamware, sasa yanabeba ahadi mpya: kwamba mustakabali wa uvuvi Kisumu ni salama zaidi, wenye nguvu zaidi, na unaowezesha maisha bora kwa wote.
Written by Laban Shikokoti