Asubuhi, maji ya mto Awaya yanatiririka kwa utulivu, lakini mioyo ya wakazi wa Obunga Mbita imejaa dhoruba ya hofu, gadhabu na matumaini yaliyopauka. Ukosefu wa daraja la kuunganisha eneo hilo na barabara ya Riat umegeuka kuwa mzigo wa maumivu kwa jamii inayosahaulika na viongozi wake, kwa sasa, daraja hilo linaonekana kama hadithi ya jini: wote wamelisikia, lakini hakuna aliyeliona!
Watu watatu wamefariki dunia, wengine wakipata majeraha mabaya, baada ya kujaribu kuvuka mto huo kwa kutumia vifaa vya kienyeji. Kwa wakazi, kuvuka mto siyo tu safari, ni mchezo wa bahati nasibu, ukishinda, unafika salama; ukishindwa, unaelekea hospitalini au kwa wazazi wa marehemu.

Wakiwa na makucha ya matumaini na nyuso za huzuni, wakazi waliandamana wakimlaumu mwakilishi wadi wa eneo hilo, Mheshimiwa Sami Onyango, kwa kulemewa na uzito wa ahadi. Walisema ametelekeza mradi ulioanzishwa na mtangulizi wake, na sasa wamedhihirisha wazi kuwa “ahadi za kampeni si kitoweo.” Wamempa makataa ya miezi mitatu, ama aanze ujenzi wa daraja hilo, au maandamano yatamng’atua afisini kama panya kwenye stoo ya unga.
“Mwenzangu alidhani kutumia magogo kuvuka ni wazo la maana. Alifika upande wa pili, lakini alikuwa tayari ameumia kwa kuunguaka kwenye haya maji, si hata unaona yako na rangi ya bluu, hi ni hatari kwa wamama na watoto,” alisema mkazi huku akicheka kwa huzuni. “Maji haya yana kiburi, hayaangalii una degree au diploma,” aliongeza mama mmoja aliyebeba mtoto na matumaini ya kesho bora.
Daraja hilo linatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha kufikia Riat, halafu Kakamega. Bila daraja, biashara zimeyumba, watoto wanakosa shule, na wagonjwa wanachelewa hospitali. Hii siyo tu changamoto ya miundombinu, ni tishio la maisha na mustakabali wa jamii.
Wakazi sasa wanatumai kuwa sauti zao zitavuka mto bila kuanguka. Familia tatu tayari zinalia kwa wapendwa walioaga dunia , na wengine wakiuguza majeraha na hisia. Kisumu ni jiji la maziwa, lakini Obunga Mbita ni kisiwa cha machozi.
‘’Tutafika tu kama daraja litajengwa, not by miracle, but by action’’ Alisema mkazi mmoja . Kwa sasa, maombi yanapanda juu, maandamano yanaongezeka, na matumaini yananing’inia kwenye nyaya za siasa za Kisumu.