Katika ufuo wa Arongo, ulioko ndani ya Eneo Bunge la Seme, Kaunti ya Kisumu, wavuvi wanalalamika kutokana na kuongezeka kwa visa vya utovu wa usalama ndani ya Ziwa Victoria. Hali hii imesababisha hofu na taharuki miongoni mwa jamii ya wavuvi, huku makundi ya maharamia wakidaiwa kuendesha unyang’anyi na uporaji wa samaki na vifaa vya kuvulia.
Wavuvi wanasema kuwa mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa watu wasiojulikana yamewatatiza pakubwa, na sasa huchukulia kila safari ya majini kama hatari kwa maisha yao. Mbali na kupoteza samaki waliovuliwa, pia hukumbwa na hasara ya mitumbwi, nyavu, na vifaa vingine muhimu vinavyotumika kwa shughuli za uvuvi.
“Tunapovua samaki usiku, maharamia hutuvamia kwa ghafla na kutupora. Mara nyingine hutulazimisha kuruka majini ili kuokoa maisha,” alisimulia mmoja wa wavuvi kwa huzuni.
Katika harakati za kuimarisha usalama na ustawi wa wavuvi, mwanzilishi wa Wakfu wa Jiwo Mwanadada Foundation, Beatrice Amondi, alifanya ziara rasmi katika ufuo huo na kukabidhi jozi za waokoaji (life jackets) kwa wavuvi. Hatua hiyo imelenga kuhakikisha kuwa iwapo maafa yatatokea ndani ya ziwa, wavuvi hawa wataweza kujinusuru.

Akihutubia umma iliyokusanyika kwa heshima ya tukio hilo. Amondi aliitaka serikali, hususan Wizara ya Uchumi wa Rasilimali za majini, kutambua mchango wa wavuvi hawa kwa uchumi wa taifa na kutekeleza mikakati madhubuti ya usalama.
“Wavuvi hawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa ziwa letu. Bila hatua madhubuti, tunahatarisha sio tu riziki bali maisha ya watu,” alisema Amondi.
Kutokana na ukosefu wa usalama, shughuli za uvuvi zimepungua, hali ambayo imeathiri moja kwa moja mapato ya jamii nyingi zinazotegemea uvuvi. Wakati baadhi yao wanatafuta kazi mbadala, wengine wanalazimika kuhama maeneo yao ya asili kwa hofu ya kuendelea kushambuliwa.
Kwa sasa, wavuvi wa Arongo wanatumai kuwa sauti zao zitafika serikalini, na kuwa serikali itachukua hatua za dharura kuimarisha ulinzi, kuboresha miundombinu, na kudhibiti shughuli haramu zinazofanyika ndani ya Ziwa Victoria.