Hofu imezidi kutanda katika kijiji cha Simotwet, Kaimugul, eneo bunge la Mlima Elgon kaunti ya Bungoma, baada ya kupatikana kwa mwili wa mwanamume aliyekatwa shingo Jumapili usiku.
Tukio hili la kutisha limewaacha wakazi wengi wakiwa na hofu na mshangao, wakitoa wito kwa asasi za usalama kuingilia kati mara moja na kubaini chanzo cha mauaji haya ya kinyama.
Kulingana na wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Patrick Chemosit, ukosefu wa usalama umechangiwa pakubwa na kukosekana kwa chifu kwa zaidi ya miaka sita sasa. Wamemtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kituo cha polisi kinajengwa haraka eneo hilo ili kuimarisha doria na kuzuia visa vya uhalifu.
“Two Weeks ago kuna Pastor aliuliwa pale Kimalewa and there is nobody who is asking about the security of this area. It is a very big concern to the people of Mt Elgon that we have a very big security lapse.”Chemosit alisisitiza.
Chemosit amesema kuwa Idara ya Usalama Mlima Elgon sasa Maafisa wa Polisi wameshika doria kulinda Mkuyu wenye utata katika kijiji cha Toroso ambapo wazee wa eneo hilo wamekuwa wakitaka kuung’oa kwa tambiko.
“Wakati ambao tunaongea hivi,the government has mobilised machinery,maaskari wote wamepelekwa kuchunga miti kule Toroso…Asubuhi utaona ng’ombe wameibwa.”Chemosit alizidi kueleza.
Katika tukio jingine, kijiji cha Cherubei Kongit wadi ya Kaptama, kimetikiswa na mauaji ya msichana ambaye mwili wake ulipatikana kando ya barabara ukiwa na majeraha mabaya.
Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi wa kina kubaini kiini cha visa hivi viwili vya mauaji, huku wakiwahakikishia wakazi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
By Wanji Sostine