Rais William Ruto ameondoka nchini Jumatatu usiku kwa ziara ya kikazi nchini Uchina, akiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa haya mawili katika biashara, uwekezaji na muundo msingi.
Ziara hii inafuatia maafikiano ya ushirikiano baina ya Kenya na Uchina mwaka 2017 ambapo Kenya ni mshirika muhimu katika msaada ya Belt and Road Initiative (BRI) Barani Afrika. Kenya imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya muundo msingi kupitia miradi kama Reli ya Kisasa SGR na Barabara ya moja kwa moja yaaani Nairobi Expressway ambayo imechangia ukuaji wa uchumi na kubadilisha madhari ya jiji.
Wakati wa ziara hiyo Rais Ruto anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Xi Jinping ili kuendeleza malengo ya pamoja katika maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa.
Rais pia atafungua rasmi Kongamano la Kibiashara la Kenya na Uchina, jukwaa ambalo linatarajiwa kuzileta pamoja kampuni 100 kutoka mataifa hayo mawili kwa lengo la kupata fursa mpya za uwekezaji, ukuaji wa viwanda na ubunifu wa kidijitali.
Katika hatua ya kimkakati ya kukuza mauzo ya mapato yanayotokana na sekta ya kilimo kutoka Kenya, Rais atazindua kituo uuzaji wa majani chai ya Kenya nchini humo cha Kenya Tea Holding katika Mkoa wa Fujian moja ya maeneo yanayoongoza katika uzalishaji wa chai nchini humo.
Kituo hiki kinalenga kupanua soko la chai ya Kenya Nchini Uchina, kuwafikia wakulima wadogo-wadogo na kuimarisha mapato yao.
Rais Ruto pia atatoa hotuba kwa wataalam na viongozi katika Chuo Kikuu cha Peking, ambapo atashiriki mazungumzo kuhusu maono ya Bara Afriika kuhusu maendeleo ya pamoja, uongozi imara na ushirikiano.
Ziara hii inatarajjiwa kuendeleza ushirikiano wa BRI unaoendana na malengo ya maendeleo ya Kenya, ukiangazia zaidi kujengwa kwa eneo la viwanda na muundo msingi wa usafirishaji Afrika Mashariki.
Kando na hayo, Rais Ruto anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Uchina kuhusu masuala ya kiamtaifa na ya kikanda, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa mataifa katika kuleta amani na kuimarisha usalama katika eneo la Pembe ya Afrika na maeneo ya Maziwa Makuu.