Kundi la Maaskofu wa madhehebu mbalimbali katika Eneo Bunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kutoa kipande cha ardhi kwa ujenzi wa kituo cha huduma kwa waathiriwa wa dawa za kulevya.
Kulingana na viongozi hao wa kidini, visa vya uhalifu maeneo hayo huenda vikapungua, kwani vijana wengi wanaojihusisha na uhalifu wamebainika kuwa waraibu wa mihadarati.
Wakizungumza na Radio 47, wakiongozwa na Mwenyekiti wao Askofu Elius Karisa, wamesisitiza kuwa kanisa haliwezi kufumbia macho ongezeko la vijana wanaopoteza mwelekeo kutokana na uraibu wa mihadarati, wakitoa wito kwa viongozi wa kisiasa, mashirika ya kijamii na serikali kushirikiana na kuweka mikakati ya kukabili janga la hilo.
“Tunaiomba serikali kutoa shamba kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kuwasaidia watoto wetu wa kike na wa kiume, ambao wamelemewa sana na mihadarati.” Mwenyekiti huyo alisema.
Askofu Levis Juma aliongeza kwa kusema kuwa, ” eneo la Jomvu lina waraibu wengi wa mihadarati. ujenzi wa kituo cha marekebisho kitafaa. Maana wanapokuwa katika hali ya uraibu wanaweza kuzama katika vitendo vya uhalifu na ukiukaji wa maadili, mambo ambayo huwa magumu kusuluhisha”
Maaskofu hao wana imani kuwa kudhibiti matumizi ya mihadarati kutasaidia pakubwa katika kupunguza visa vya uhalifu maeneo hayo, kwani vijana wengi wanaotumia mihadarati na kufanya uhalifu wanasingizia ukosefu wa ajira kama sababu kuu, ili wapate kipato.
Asasi za usalama Ukanda wa Pwani zimekuwa mbioni kuyakabili magenge ya wahalifu, yanayotumia panga kama silaha, maarufu “panga boys” wanaowateka watu na kuwaibia kwa mabavu.
Vita dhidi ya mihadarati pia imekuwa ikiendelea katika Kaunti ya Mombasa, serikali ya kaunti hiyo ikipiga marufuku matumizi ya mugukaa mnamo mwezi Mei mwaka 2024, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, akisisitiza kuwa matumizi ya mugukaa yanasababisha madhara ya kiafya.
Mbali na hayo, maaskofu kutoka Jomvu wamelalamika kuwa ardhi nyingi zilizojengwa kanisa eneo hilo hazina hatimiliki, na hivyo kuitaka wizara inayohusika kutoa hatimiliki hizo.
Wito huu umetolewa na Askofu Peter Menza “Tunahitaji mchakato wa utoaji hatimiliki eneo hili kuharakishwa, hasa katika ardhi zilizojengwa makanisa. Hilo ndilo jambo ambalo tunataka kusisitiza ili tuweze kumiliki ardhi hizo bila wasiwasi wa kufurushwa ama mashamba hayo kunyakuliwa.”
Mshauri wa Rais wa Maswala ya Kisiasa Karisa Nzai, alikutana na viongozi hao wa kidini na kutoa ahadi kwamba matakwa yao yataangaziwa, huku akihimiza ardhi hizo kununuliwa na hatimiliki kutolewa, chini ya mpango wa kumaliza uskuota Pwani, ambapo Rais William Ruto aliahidi kiasi cha shilingi bilioni moja ili kufanikisha mpango huo.
“Ninawahimiza wanaohusika katika mpango huu kuhakikisha ardhi zilizojengwa maeneo ya kuabudu zinanunuliwa” hatahivyo, nawaomba maskuota kuondoa wasiwasi kwani mpangilio wa rais Ruto uko imara”
Written by, Paul Muniu