Hafla ya mazishi katika kijiji cha Lwandeti, eneo la Matete, Kaunti ya Kakamega, yaligeuka kuwa uwanja wa vurugu baada ya waombolezaji kumvamia mhubiri aliyekuwa akiendesha ibada, wakimshutumu kwa kuendesha ibada hiyo kinyume na mila na desturi za jamii hiyo.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, hali ya taharuki ilianza baada ya mhubiri huyo kumzuia mzee Joseph Wafula baba mzazi wa marehemu kutoa risala katika hafla ya mazishi ya mwanawe, Kitali Kundu.

Kitendo hicho kilionekana kama dharau kwa familia, na kilichochea hasira miongoni mwa waombolezaji.

“Kulingana na ratiba ya mazishi, nilikuwa nimepangiwa kutoa risala kama mzazi wa marehemu. Lakini mhubiri alikataa, akasisitiza kuwa ni mama mjane pekee ndiye anayepaswa kuhutubia waombolezaji,” alisema Mzee Joseph Wafula, baba mzazi wa marehemu.

“Hili halikukubalika kwa mila na desturi zetu, kwani katika jamii yetu, mkaza mwana hastahili kuzungumza mbele ya wazazi wa marehemu. Hapo ndipo waombolezaji walipopandwa na hasira na kusema kuwa, iwapo babake marehemu hataongea, basi mhubiri huyo hastahili kuendesha ibada ya mazishi,” aliongeza.

Taarifa zinasema kuwa mzozo huo ulifikia kilele wakati mhubiri huyo aliposimama juu ya kaburi la marehemu na kuanza kutoa laana dhidi ya familia hiyo, akidai kuwa kifo cha kijana huyo kilitokana na laana ya kifamilia na kutotubu dhambi.

Kauli hizo, zilizodaiwa kuwa za kuudhi na zisizokuwa na heshima, ziliwakera waombolezaji waliomvamia kwa ghadhabu, wakimshambulia hadharani.

“Pasta alipanda juu ya kaburi na kuanza kulaani familia ya marehemu. Hilo liliwakera sana waombolezaji, ambao kwa hasira walimfukuza na kuamua kumzika jamaa yao bila usaidizi wa kanisa, wakisema kuwa mhubiri huyo alikuwa akikiuka mila na desturi za jamii. Ukienda Roma fanya yawaroma,” alisema mmoja wa waombolezaji aliyehudhuria mazishi hayo.

Kwa ghadhabu na hasira, waombolezaji walimvamia mhubiri huyo na kumshambulia vikali, huku vipaza sauti vya kanisa vikiharibiwa.

Baadaye, walimtimua kabisa kutoka eneo la mazishi, na familia ikaamua kuendelea na shughuli za kumzika mpendwa wao bila usaidizi wa kanisa.

Kulingana na mzee wa mtaa, Moses Naibei Masai, tukio hilo linaonyesha ongezeko la mvutano kati ya baadhi ya makanisa na jamii za mashinani, hasa pale kanisa linapopuuza au kudharau mila za wenyeji.

“Mazishi ni sehemu muhimu ya kutoa heshima za mwisho kwa wapendwa wetu. Ni lazima kuwepo kwa ushirikiano wa heshima kati ya kanisa na jamii. Iwapo maelewano hayo yatakosekana, migogoro kama hii itaendelea kujitokeza. Dini na tamaduni za asili lazima ziwe na uhusiano wa kuelewana,” alisema Masai.

Tukio hili limeibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya makanisa katika shughuli za kitamaduni, huku baadhi ya viongozi wa kijiji wakitaka kuwe na mafunzo kwa viongozi wa kidini kuhusu namna ya kuhudumu katika mazingira yenye tamaduni tofauti.

Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa kanisa husika kuhusu tukio hilo, huku familia ya marehemu ikisisitiza kuwa haitarajii kushirikiana tena na viongozi wa dini waliovuruga ibada hiyo ya mazishi.

Story by Violet Auma.