Serikali itachukua hatua kali dhidi ya wale watakaopatikana na hatia katika uchunguzi unaoendelea kuhusu madai ya ulanguzi wa binadamu nchini.
Waziri wa Usalama na Masuala, Kipchumba Murkomen, ameahidi kuwachukulia hatua wote watakaohusishwa katika uchunguzi unaofanywa na kuchukua hatua kulingana na mapendekezo ya jkamati maalum iliyobuniwa na Waziri wa Afya, Aden Duale.
Murkomen alisema kwamba ingawa wizara yake inafuatilia kwa karibu suala hilo, huduma ya matibabu ya upandikizaji wa viungo ni taaluma maalum inayosimamiwa na idara maalum kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.
Akiwahutubia wanahabari mjini Machakos Murkomen alisema, “We will be guided by the report of the oversight agencies like the KMPDU and others on the way forward and those found culpable will be dealt with as per the law.”
Katika siku ya mwisho ya ziara yake katika eneo la Mashariki wakati wa mkutano wa washikadau wa usalama kwa jina Jukwaa la Usalama katika Kaunti ya Machakos, Murkomen alithibitisha kuwa wizara yake itachukua hatua mara tu malalamiko rasmi yatakapowasilishwa.
“If the specialized agencies reveal that there were transgressions, widespread anomalies or areas of fraud, the long arm of the law will not spare anyone irrespective of their status in society,” Alisema Murkomen.
Kadhalika, aliipongeza hatua ya Waziri wa Afya Aden Duale kuunda jopo kazi la kuchunguza suala hilo na kutoa mapendekezo ya hatua zinazofaa kuchukuliwa.
Alifichua kuwa wizara bado haijapokea malalamiko kuhusu suala hilo, lakini aliahidi kulifikisha kwa polisi na mashirika yanayosimamia sekta hiyo mara litakapopokelewa.
Ni ijumaa ambapo Waziri Duale alizindua kamati maalum itakayochunguza sakata ya ulanguzi wa viungo vya binadamu nchini.
Kamati hiyo ya watu kumi na watatu ina miezi mitatu kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti.