Familia Moja katika eneo la Mwakitau, Eneo Bunge la Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta imefukua mwili wa mpendwa wao Mchungaji Edward Maghanga aliyezikwa kule Vindo eneo Bunge la Voi.
Tukio hili limefanyika jioni ya umatatu tarehe 28 na limechukua muda wa saa nne.
Kifo cha Mwanamume huyo anayeaminika kuwa Mchungaji katika eneo la Voi, anasemekana kufariki dunia kwa njia ya kutatanisha na kuzikwa upesi na kinyume cha mapenzi ya familia yake ambayo imetofautiana na Mke wa Mchungaji huyo ambaye awali alisema amemzika mumewe kulingana na mapenzi yake alipokuwa hai.
“Nimekuja hapa nikaambia watoto wangu wamfukue mtoto wangu Edward niende naye Mwakitau, mimi ndio nimewapatia ruhusa na kama nikushikwa nije nishikwe mimi, lakini mtoto wangu nataka nende naye Mwakitau.” Alielezea Mamake Edward kwa huzuni.
Tofauti hizo aidha zilisababisha familia ya Edward Maghanga ikiongozwa na Mama yake mzazi Hanna Maghanga kwenda mahakamani kudai haki ya mwanao na kuomba idhini ya kumfukua ili kuenda kumzika kwao nyumbani.
Kadhalika, Wanafamilia hao walifika katika Mahakama ya Voi kusikiliza maamuzi ya ombi la kumfukua na badala yake wakapata habari kwamba kesi imeamuliwa mtandaoni (online) kwa ghadhabu wakaamua kumfukua kutokana na amri ya mazazi.
“Tumekuja mahakamani saa mbili tuka kaa hadi saa nane tukisubiri, tukiulizia tunaambiwa kesi yenu ilipita kitambo na hatujaitwa.” Alalamika mwanafamilia.
Wakati uo huo, wamelalamikia kunyimwa haki kwa kuahirishwa kwa kesi hiyo ambayo kwa matarajio yao walipendelea uamuzi utolewe mara moja na kuruhusiwa kuufukua mwili wa Edward Maghanga.
“Serikali hawajatusikiza kilio chetu, hatujafanyiwa haki yoyote, Mahakama ya Voi haijatutendea vyema, watawekaje kesi ‘online’ na sisi hatujaambiwa twende kusikiza na badae wanatuambia ati kesi imeahirishwa hadi tarehe 16 mwezi wa 6, hiyo mwili si itakua inaoza?” Alisikitika Jane Mwalimo.
Kutokana na hatua familia hiyo kuchukua sheria mikononi mwao sasa wanatarajia kuuzika mwili wa Edward Maghanga nyumbani kwao eneo la Mwakitau, Mwatate Kaunti ya Taita Taveta jumanne tarehe 29 mwezi wa 4.
Haya yote yamefanyika bila kuwapo kwa afisa yeyote wa Usalama ila Familia ya Hannah Maghanga tu.
Written by, Julius Mariki