Siku chache tu baada ya kurejea nchini kutoka Marekani, aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i amejiunga rasmi na viongozi wa upinzani. Matiang’i amefanya mkutano Jumanne asubuhi Aprili, 29 na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa People Leberation Party, Eugene Wamalwa wa DAP-K, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi ,Mukhisa Kituyi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.
Gachagua amemkaribisha Matiang’i katika muungano huo akiutaja kuwa utakaolikomboa taifa. Gachagua amesema ”The team to liberate Kenya gets bigger every day. Welcome, Dr. Fred Matiangi, Hon. JB Muturi and Hon. Mithika Linturi.” Gachagua aliendelea na kusema ”You are on the right side of history.”
Ikumbukwe Gachagua amekuwa akishinikiza muungano wa upinzani ulio imara akisema ndio utamshinda Rais Ruto, 2027
Kupitia mitandao yake ya kijamii Kalonzo amemkaribisha Matiang’i akisema ”A very good morning and welcome onboard. This is the Team that will komboa Kenya.”
Japo yaliyojadiliwa katika mkutano huo hayajawekwa wazi, inaaminika kuwa viongozi hao wanapanga mikakati ya ushirikiano kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.
Tangu kuwasili nchini Matiang’i anasemekana kuwa amekuwa akifanya mikutano na viongozi mbalimbali hasa wale wa kijamii ikizingatiwa kuwa wapo wanamsukuma aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kuwania pia urais.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni ambaye amekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Matiang’i na hata kutangaza kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hicho hakuwa katika mkutano huo.
Kioni ni miongoni mwa viongozi waliomkaribisha Matiang’i alipowasili nchini kutoka Marekani wiki mbili zilizopita.
Matiang’i aliyekuwa na usawishi wakati wa serikali ya Uhuru Kenyatta amekuwa akipigiwa upatu kuwania urais mwaka 2027.
Japo mwenyewe hajatoa msimamo kuhusu nia yake ya kuwania wadhfa huo, wandani wake wanaamini kuwa anatosha kumenyana na vigogo wengine wa kisiasa, 2027.