Seneta wa Nandi Samson Cherargey ameilaumu idara nzima ya usalama kufuatia vifo vya watu watano katika eneo la Angata Barrikoi, Trans Mara Kaunti ya Narok.

Akizungumza Jumatano Aprili tarehe 30, siku moja tu baada ya maafisa wakuu katika eneo hilo kuhamishwa, Cherargey hasa anailamu Idara ya Ujasusi NIS akisema ilizembea kwa kutotoa taarifa mapema kuhusu matukio ambayo yalishuhudiwa Jumatatu, ambapo watu watano walipigwa risasi na kuuliwa na maafisa wa polisi.

Cherargey aliuliza, ‘’Na pia nataka Idara ya Ujasusi ya NIS, by the time hawa watu, maafisa wa survey  walienda ground. Hawa NIS walikuwa wanafanya nini wasijue kulikuwa na hali ya mishike mishike, ndio wasizuie hawa watu waende katika mashinani.’’

 Cherargey amesema idara zote za usalama zinatengewa bajeti kubwa hivyo zinafaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

‘’Hizi vyombo ya usalama tunawapea pesa nyingi katika bunge kwa mfano wale NIS tuliwaongezea 6bilion ndio wafanye kazi mzuri.’’ Alisema Cherargey.

Wakati uo huo, seneta huyo amewashauri maafisa wa polisi kutekeleza majukumu yao kulingana na sheria na kutokubali kufuata amri ambazo zinaweza kuwatia mashakani baadaye.

Alisema hivi, ‘’Mimi nataka kusema hawa maafisa wa polisi wanafanya kazi mzuri, lakini jua ziku ile utakiuka ama utafuata amri ya mdosi wako ambaye haiambatani na sharia siku ile utashikwa, utashikwa  peke yako.’’

Aidha amewataka maafisa hao wa polisi kutotumia risasi kuwatawanya waandamanaji.

‘’Pia nataka kuwaambia hao polisi wasitimie live bullets, wangetumia, rubber bullets, wangetumia maji ama hata teargar’’ Alisisitiza.

Ameshtumu hali ya maafisa wa polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji wasio la silaha akisema ‘’unapiga aje risasi Mkenya ambaye hana kitu kwa mkono? You know we need to be fair in this country na hii ni miaka 63 baada ya uhuru.’’

Zaidi ya hayo amesema sharia inafaa kufuata mkondo wake wakati wananchi wanapofanya makossa akisema wangekamatwa na kufunguliwa mashtaka ‘’Polisi hawakuwa na sababu yoyote ya kuwapiga risasi na kuwaua, kuna kushikwa kuna kufunguliwa mashtaka’’ alisema Cherargey.

Hayo yakijiri, amezitaka idara zinazohusika kama ile ya Mkurugenzi wa Mashataka ya Umma kuharakisha uchunguzi ili waliohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua za kisheria.