Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi COTU, Francis Atwoli, amemshauri Rais William Ruto kutoyumbishwa na kauli zinazoendelea dhidi yake ikiwamo ile ya ‘Ruto Must Go’.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Siku ya Leba yaliyofanyika katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi, Atwoli alisema kuna watu wanaolalamika bila msingi wowote, akisisitiza kuwa Rais anastahili kupewa nafasi ya kukamilisha muhula wake wa uongozi.

“Hawa Wakenya unasikia wanasema ‘ground ni mbaya’, lakini huyo anayesema hivyo hana hata ground. Mtu apewe nafasi amalize kazi yake,” alisema Atwoli wakati wa hotuba yake.

Katibu huyo pia alitumia jukwaa hilo kutetea msimamo wa COTU wa kushirikiana na serikali iliyoko madarakani, akieleza kuwa jukumu la muungano huo ni kulinda maslahi ya wafanyakazi, si kushiriki siasa.

“COTU si chama cha kisiasa. Tunahudumia serikali iliyopo madarakani kwa niaba ya wafanyakazi. Sisi ni sauti ya wafanyakazi, sio wanasiasa,” alifafanua Atwoli.

Katika hatua nyingine, Atwoli alirejelea wito wake wa kudhibiti mitandao ya kijamii nchini, akionya kuwa matumizi mabaya ya majukwaa hayo yanaweza kusababisha machafuko.

‘ I am appealing to Kenyans, we must love this country; we have no any other country, if the this country went down to the dogs we have no any exit route.” alisema Atwoli. Aliendelea na kusema ”One Day you Kenyans will remember me. If we don’t regulate social media, in China with over 1.4 bilion people, Dubai, United States of America social media is regulated, Kenya cannot be free.” alihoji kwa msisitizo.

Kauli za Atwoli zinajiri wakati ambapo mijadala mikali imekuwa ikiendelea katika mitandao ya kijamii kwa muda mrefu dhidi ya Rais Ruto.

Ni mijadala ambayo imewaweka baadhi ya vijana katika njia panda wengi wakijipata mbele ya mahakama kwa kumkejeli na kumkosea heshima Rais Ruto. Kwa mfano, kisa cha Mkenya Sifuna aliyeshtakiwa kwa kutumia akaunti ya X kwa jina ”Must Go” ikiwa na picha ya Rais kueneza jumbe zisizofaa kwa Rais na familia yake.