Mashindano ya magari ya Equatorial Classic Rally 2025 yameanza rasmi katika Kaunti ya Taita Taveta, Alhamisi asubuhi, yakilewata pamoja madereva 19 wakiwamo wanne wa kimataifa.
Mashindano hayo ya siku tatu yalizinduliwa rasmi na Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime na Naibu wake Christine Kilalo, wakiandamana na maafisa wengine wakuu katika serikali ya kaunti wakiongozwa na Katibu wa Kaunti Friday Mwafuga miongoni mwa wengine na Waziri wa Vijana na Michezo Shadrack Mtungi na Getrude Shuwe wa Biashar.
Shughuli hiyo aidha inatarajiwa kufanyika katika umbali wa zaidi ya kilomita 628 katika shamba za Jamii na lile la Mkonge la Teita Estate ambapo,gari zimeratibiwa kuanza eneo la Club Hoteli kisha kuelekea Kamtonga, Lumo, Bura, Maktau, Mariwenyi, Pusa kisha kurejea Club house.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya uzinduzi huo, Mratibu mkuu wa mashindano hayo Kashif Shaikh alisema wanatarajia kuwa na shughuli njema lenye mafanikio licha ya changamoto za barabara ambazo zimepelekea kupunguzwa kwa kilomita zilizokusudiwa awali.
“Mashindano yameanza rasmi. Tulikuwa na madereva 20 waliojiandikisha, lakini mmoja wa kimataifa hakuweza kufika kutokana na changamoto za usafiri. Kwa sasa tuna madereva 19, na leo pekee wanatarajiwa kushindania kilomita 268,” alisema Shaikh.
Miongoni mwa magari yanayovutia ni Mini Cooper ya cc 1300, ndogo kuliko yote katika mashindano haya, inayoweka ladha ya kipekee ya kihistoria katika ushindani huo. Mashindano haya yamewavutia mashabiki wa magari kutoka ndani na nje ya nchi, kwa mchanganyiko wa magari ya kizamani na yale yaliyoboreshwa kwa kasi.


Ili kuhakikisha usalama na uratibu wa mashindano, Shaikh alieleza kuwa zaidi ya waamuzi 100 wamewekwa maeneo mbalimbali ya njia, pamoja na magari maalum ya kuokoa yaliyokwama matopeni, huku polisi na walinzi wa wanyamapori kutoka hifadhi jirani wakihusishwa kikamilifu.
“Changamoto kubwa kwa sasa ni matope kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni. Hata hivyo tumejipanga vyema. Tuna magari mawili yanayopita mbele ya magari ya mashindano kukagua njia, na madereva wote wameelekezwa kuwaruhusu wanyama pori kupita wanapokutana nao. Mashindano haya yanafanyika kabisa ndani ya shamba la binafsi, na uhifadhi wa mazingira ni kipaumbele,” akaongeza Shaikh.
Awali mashindano yalipangwa kufanyika umbali wa kilomita 800, lakini mvua na barabara kutopitika vililazimu waandaaji kupunguza kilomita 160, hivyo kufanikisha umbali wa mwisho wa kilomita 628.
Ukaguzi wa kiufundi na usalama wa magari ulifanyika Jumatano, ambapo madereva walifanya mazoezi kujifahamisha na njia na kurekebisha magari yao kabla ya kuanza rasmi.
Gwiji wa mashindano ya magari nchini Kenya, Ian Duncan, ambaye alihudhuria maandalizi ya kabla ya mbio, aliwapongeza waandaaji wakiongozwa na Anthony Nielsen kwa kuandaa tukio la kiwango cha juu katika eneo jipya.
“Ni jambo la kupendeza. Inasikitisha tu kwamba Anthony hatashiriki, bila shaka atatuonea wivu kesho. Lakini wamefanya kazi ya kupigiwa upato. Natumai mashindano haya yataendelea kudumu,” alisema Duncan.
Tofauti na mashindano ya kawaida, Equatorial Classic Rally haina utangulizi wa uchunguzi wa njia (recce) wala nakili za mwendo (pace notes), ikifuata mtindo wa marathon rally ambao hujaribu uwezo wa gari na akili ya dereva.
Equatorial Classic Rally inalenga kuwa tukio la kila mwaka katika ratiba ya mashindano ya magari Afrika Mashariki, na mashindano haya yanaashiria mwanzo mzuri.



Mchanganyiko wa changamoto za kiufundi, masuala ya kimazingira, na ushiriki wa kimataifa unaliweka kuwa moja ya mashindano ya kufuatilia kwa makini katika miaka ijayo.
Huku madereva wakionyesha uweledi wao haswa katika kuendesha magari kwenye njia zilizojaa changamoto na kwa kasi zaidi, lililosalia sasa ni kuona nani ataibuka mshindi mwishoni mwa mashindano haya.
Madereva kadhaa wa mashindano hayo waliozungumza na Radio47 na Tv47 dakika chache kabla ya kuanza mbio zao, walieleza furaha yao kushiriki na vilevile kufurahia mazingira na manthari shwari eneo hilo la Taita Taveta.
“Maandhari haya bila shaka ndio bora zaidi na nina furaha niko na bahati ya kuja kushiriki kutoka Uingereza, na natazamia kufurahia zaidi” alieleza Boby
Written by, Julius Mariki |