Taharuki imetenda tena katika eneo la Angata Barrikoi, Transmara Kusini baada ya watu wasiojulikana kuvamia na kuteketeza sehemu kubwa ya mashamba ya miwa.
Moto huo ambao umeteketeza ekari nyingi za mashamba ulianza kwa njia isiyoeleweka. Wakulima sasa wamesalia wakikadiria hasara kwani hakuna kilichookolewa.
Maafisa wa vitengo mbalimbali vya usalama wanachunguza tukio hilo huku wengine wakitumwa kudhibiti hali. Inaaminika huenda moto huo uliansihwa na watu waliotaka kulipiza kisasi.
Kisa hiki kinajiri siku chache tu baada ya watu watano kuuliwa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi wakati wa makabiliano baina yao walipokuwa wakilalamikia kile walichodai ni mpango wa unyakuzi wa ardhi.
Kisa hicho kiliibua hisia kali nchini hadi kusababisha Inspekta Mkuu wa polisi Douglas Kanja kuwahamisha maafisa wakuu wa usalama kutoka eneo hilo.
Aidha shinikizo zinazidi kwa idara zinazohusika kufanya uchunguzi kufahamu kiini ya mzozo wa ardhi hiyo ya ekari 6, 300 ili kuzuia visa kama hivyo siku za usoni.