Hatimaye Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2025, kuwa sheria katika hafla iliyofanyika Alhamisi, Ikulu. Rais ameitaja sheria hiyo mpya kuwa endelevu na ambayo itahakikisha watu wenye ulemavu nchini wanapata haki, kuambatana na katiba hasa akitaja sehemu ya 54.

Akizungumza baada ya kutia saini mswada huo, rais amesema sheria hiyo itahakikisha haki kama vile elimu, huduma za afya, ajira na kushirikishwa katika maamuzi ya kisiasa zinapatikana kwa urahisi kwa watu wenye ulemavu.

Seneta Crystal Asige, ndiye aliyekuwa mwasisi wa Mswada wa Watu wenye ulemavu wa mwaka 2023 , ambao ulichapishwa Februari mwaka huo.

Mswada huo ulipitishwa pamoja na marekebisho katika seneti Februari mwaka 2024, kisha ukapitishw apia katika Bunge la Kitaifa Januari, mwaka 2025.

Katika mswada huo sehemu ya 133 imeweka bayana kwamba haki za watu wenye ulemavu lazima ziheshimiwe na mtu atapokea huduma zinazostahili kulingana na hali yake ya ulemavu.

Aidha sheria hiyo inaharamisha ubaguzi wa aina yoyote kwa watu wenye ulemavu na kushinikiza maeneo yanayostahili kwa walemavu hasa katika magari ya uchukuzi wa umma, majengo na mawasiliano.

Aidha sheria hiyo inatoa mwongozo kuhusu kupunguzwa kwa kodi wanaowajiiri watu wenye ulemavu. Sio hayo tu sheria hiyo pia inasema kuwa yeyote anayekiuka haki za walemavu basi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha Baraza la Kitaifa la Kuwashughulikia Watu Wenye Ulemavu limetwikwa jukumu kuhakikisha sheria hizo zinaekelezwa.

Mswada huu unaainisha wazi majukumu ya serikali ya kitaifa na za kaunti, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sera za kitaifa kuhusu ulemavu katika ngazi ya kaunti, uundaji wa kamati za ushauri za kaunti, na hitaji la asilimia angalau tano ya nafasi zote za ajira katika serikali za kaunti kutengewa watu wenye ulemavu.

Katika elimu, Mswada huo unahakikisha mazingira jumuishi ya kujifunzia yenye marekebisho yanayoendana na mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu. Pia unataka kuwapo kwa ulinzi katika utoaji wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, pamoja na huduma hizo za afya ziwe bila malipo.