Wakazi wa eneo la Muslim mtaani Kawangware, jijini Nairobi, wamelalamikia athari kubwa za taka zinazotupwa kiholela katika eneo hilo. Wanasema licha ya kuwasilisha malalamiko yao kwa mamlaka zinazohusika, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.

‎Wakizungumza na Radio 47 Alhamisi, wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo wanasema kuwa taka hizo ambazo zimesalia hapo bila kuondolewa kwa muda mrefu, zimeziba mitaro ya kupitisha  maji taka, na kunaponyesha maji taka huingia hadi kwenye nyumba zao, hali ambayo imesababisha wengi wao kupatwa na magonjwa mfano kipindupindu na homa ya mapafu TB.

‎Aidha wafanyabiashara wameelezea huathirika pakubwa kibiashara huku wakikosa wateja kutokana na taka hizo ambazo zimeziba barabara.

‎”Biashara zetu zimerudi chini. Sasa hivi wateja hawakuji kwa sababu barabara ya kuingia kwenye maduka yetu zimezibwa na takataka na harufu mbaya inayotoka katika kwenye takataka hizo,” alisema Grace Muthoni.

‎Kulingana na Kasisi Aggrey Muambe ambaye kanisa lake linaelekea kufunikwa kutokana na taka hizo, anasema kuwa barabara ya kuingia kwenye Kanisa hilo iimezibwa hivyo kuwa vigumu kwa waumini wake kuingia kanisani. 

‎” Tayari waumini wangu watatu wanaugua. Sasa wako nyumbani wakiendelea na matibabu. Hawajaja kanisani kwa miezi kadhaa sasa. Hapa harufu utawala hata kutoa mahubiri huwa vigumu sana,”  Alisema kasisi Muambe.

‎‎Si wafanyabiashara pekee walioathririka kutokana na taka hizo bali pia wanafunzi wa shule ambazo ziko karibu na jaa hilo pia wameathirika hata zaidi. Kulingana na wakazi wanafunzi huibiwa wanapopita katika mtaa huo, kwani taka hizo huwavutia wezi na wahalifu pia. Wanasema kuwa kuna baadhi ya akina mama ambao wamebakwa walipokuwa wakipita sehemu hiyo huku wengine wakiibiwa.

‎Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi kuwajibika na kuzoa taka hizo ili wakazi na wafanyabiashara waishi kwa amani la sivyo waandamane.

‎Suala la taka limekithiri sana jijini Nairobi. Kwenye mitaa mingi hasa ya mabanda taka zimetupwa kiholela ila hakuna anayeshughulika mfano Kawangware mtaa wa Msalaba, Kibera eneo la Woodley, Kangemi kwa soko na maeneo mengine.

‎Written by, Silas Kemboi