Pana haja ya serikali ya kitaifa pamoja na zile za kaunti kushirikiana katika kampeni za kuwahamasisha vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kwa ajili ya kuwa na kizazi bora siku sijazo 

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya kukabili matumizi mabaya ya pombe (NACADA) Stephen  Mairori akizungumza katika Kanisa la AIC Ikutha Kitui Kusini,ameelezea kusikitika kwake kuwa asilimia Kubwa ya vijana hasa katika vyuo vikuu wanatumia mihandarati,hali inayotishia maisha yao ya baadaye. Anasema kuwa kama hatua za haraka za kudhibiti pombe haramu na dawa za kulevya miongoni mwa vijana hazitachukuliwa,huenda nchi ikakosa kuwa na viongozi bora siku za usoni.

“Ile sehemu tunapaswa kuzingatia sana ni vijana wetu. Kulingana na utafiti tuliofanya hivi karibu unaonesha kuwa karibu nusu ya vijana katika vyuo vikuu wanatumia pombe na dawa za kulevya na hiyo ni hatari sana.Tunaweza kujenga barabara,tukafanya maendeleo mengi lakini kama hatutakuwa na watu wako sawa kuendesha nchi,itakuwa ni shida Kubwa,”aliongezea Mairori 

Aidha maeneo yote ya burudani ambayo yamekIuka sheria za kudhibiti pombe haramu,yatafungwa mara moja na kupokonywa leseni za kuhudumu. Amesema oparesheni za vilabu ambavyo vimekeuka sheria inaendelea,na kuwa wote watakaopatika na hatia watawajibishwa Kisheria na leseni zao kufutuliwa mbali.

“Wale ambao wako na leseni kuna wengine unapata wako sawa,lakini maafisa wetu wakitoka hivi tu,wanaleta nyingine mbaya. Tunawaonya kuwa  leseni zao zinachukuliwa na maafisa wa serikali ya kitaifa hata bila kuzingatia leseni walizopewa na serikali za kaunti,hila serikali ya kitaifa na za kaunti zinafanya pamoja ili kuhakikisha sheria zinafuatwa,”alisisitiza 

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya serikali ya Kaunti ya Kitui kuzindua kamati ya watu saba katika kila eneo bunge ili kutathmini hali ya vilabu na kutoa ripoti yake kila mwezi,katika juhudi za kukabili pombe haramu.

Vilabu vyote ambavyo vitapatikana vimekiuka sheria pamoja na zenye ziko karibu na shule,makanisa nmiongoni mwa maeneo mengine yanayohatarisha maisha ya vijana, vitafungwa mara moja na leseni zao kufutuliwa mbali.

Aidha serikali ya kaunti ya Kitui i mbioni kujenga Kituo cha urekebishaji tabia  katika eneo la Ikutha kwa vijana ambao tayari wametokomea katika urahibu wa dawa za kulevya.