Viongozi wanazidi kukosoa vikali hatua ya kuhangaishwa kwa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere wakati wakijitayarisha kuigiza mchezo wa ‘’Echoes of War’’ katika Tamasha la Kitaifa la Drama awamu ya mwaka huu.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Justin Muturi ameibua maswali kuhusu ni kwa nini serikali inawahangaisha wanafunzi na kuwanyima haki zao. Amesema ni unafiki kwa serikali kuendelea kuzungumzia masuala ya demokrasia ilhali inawanyanyasa wananchi wake.

Wakati uo huo, baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua wamedai hatua hiyo imetokana na mwandishi wa mchezo huo Cleophas Malala ambaye amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa seikali.

Wakiongozwa na Seneta wa Kiambu Karungo Thangwa na Mbunge wa Githunguri Muthoni wa Muchomba wametishia kuwaongoza wanao kuandamana kupinga uongozi wa Rais William Ruto ambao wameutaja kuwa wa ukandamizaji.

Seneta Karungo amesema matukio ya tangu Jumatano yanaonesha ukiukaji mkubwa wa haki za wanafunzi na wahusika katika sekta nzima ya Sanaa nchini.

Wamuchomba amemtetea Malala akisema amekuwa akihusika pakubwa katika Sanaa hasa kuandika michezo ya kuigiza ambayo imeshirikishwa mara si moja katika Tamasha za Kitaifa.

Wamuchomba ameunga mkono kauli ya Karungo akisema ni ukiukaji mkubwa wa katiba ambayo serikali iliapa kuilinda.

Viongozi hao wamewapongeza wanafunzi wa Shule hiyo ya Upili ya Butere kwa kusimama kidete baada ya kususia kushiriki katika Tamasha hiyo.

Mapema leo wanafunzi hao walikataa kushiriki katika Tamasha la Kiatiafa la Drama na badala yake kuimba Wimbo wa Taifa kisha kuondoka jukwaani.