Watu kumi na wawili wameaga dunia kufuatia ajali mbili tofauti zilizotokea katika kipindi cha chini ya saa ishirini na nne zilizopita. Ajali hizo zimetokea katika eneo la Limuru na Kiambu.
Katika ajali ya mapema Ijumaa watu saba wameaga dunia baada ya matatu waliyokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kuanguka kisha kubingiria mara kadhaa katika barabara ya Kamandura kwenye Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru.
OCPD wa Limuru Mary Gachie amesema ajali hiyo ilihusisha matatu iliyokuwa ikitoka Nairobi kuelekea Kijabe.
Abiria watano walifariki papo hapo na wengine wawili wakiaga dunia kutokana na majeraha walipokuwa wakitibiwa hospitalini. Majeruhi wanne waliopata majeraha mabaya wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya Tigoni.
Ajali hiyo imetokea saa mbili asubuhi, takriban kilomita moja kutoka eneo la ajali nyingine mbaya iliyotokea Alhamisi jioni.
Katika ajali hiyo ya Alhamisi watu watatu walifariki papo hapo baada ya gurudumu la gari waliyokuwa wakisafiria kupasuka. Majeruhi wengine wawili walifariki dunia walipokuwa wakitibiwa.
Mabaki ya magari yaliyohusika katika ajali hizo yamepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Tigoni.