Daktari Mercy Mwangangi ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Dkt. Mwangangi ambaye ni mtaalamu wa afya ana uzoefu wa zaidi ya miaka kumi na mitano katika masuala ya bima ya afya kwa wote (UHC), mageuzi ya taasisi, na uimarishaji wa mifumo ya afya. Katika uteuzi huo Wazri wa Afya, Adan Duale amemtaja Mwangangi kuwa kiongozi aliyebobea katika uongozi wa sekta ya afya, kwani ana rekodi ya mafanikio katika mageuzi ya sera na ufadhili wa afya nchini .
Kwa sasa, Dkt. Mwangangi ni Mkurugenzi Mkuu wa Uimarishaji wa Mifumo ya Afya katika shirika la AMREF Health Africa, ambapo ameongoza uwekezaji katika ufadhili wa afya na usalama wa afya barani Afrika, pamoja na kupata misaada ya maendeleo kwa huduma ya afya ya msingi na upanuzi wa UHC.
Duale amesema Daktari Mwangangi ana uwezo wa kuongoza taasisi hiyo mpya na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Uteuzi huu umefanyika baada ya mchakato wa ushindani wa watu 92 waliotuma maombi, ambapo 12 waliorodheshwa na kuhojiwa.
Ikumbukwe, Mwangangi alihudumu katika wadfa wa Afisaa Mkuu wa Utawala wa Wizra ya Afya chini ya Utawala wa serikali ya Jubilee.
Wakati wa muhula wake alihusika katika uundaji na utekelezaji wa mpango wa majaribio wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC) chini ya Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee.