Watu 3 wa familia moja wameteketea kiasi cha kutotambuliwa kufuatia mkasa wa moto uliotekeza nyumba walioyokuwa wamelala Jumamosi alfajiri kwenye Lokesheni ya Kibuk, eneo la Mlima Elgon, katika Kaunti ya Bungoma.

Kulingana na baadhi ya majirani mkasa huo umetokea saa kumi na moja alfajiri. Mmoja wa majirani kwa jina Dominic Ngeiyo, juhudi za wakazi kujaribu kuuzima moto huo ziliambulia patupu kwani moto huo ulikuwa ukisambaa kwa kasi.

”Majirani tulisikia hii mkasa na tulipofika moto ulikuwa umetapakaa sehemu zote, tulijaribu lakini hatukuweza, na sasa vile unaona mama na wajukuu wake wawili wameangamia.” aliyesma Ngeiyo.

Ngeiyo amelalamikia ukosefu wa wazima moto katika Kaunti Ndogo ya Mlima Elgon akisema hilo limekuwa tatizo kubwa kwani si mara ya kwanza, watu wanafariki dunia kutokana na mkasa wa moto.

Wakati uo huo, amelalamikia muundo msingi duni akisema barabara za maeneo ya mashinani ni mbovu hali inayofanya shughuli za uokoaji kuwa ngumu.

Mkazi huyo aidha ameibua madai kuwa eneo hilo limebaguliwa nakimaendeleo akimtaka Gavana Ken Lusaka kutekeleza miradi ya maendeleo katika eneo hilo sawa na ilivyo katika maeneo mengine ya Kaunti.

”Unajua hapa hata barabara ni mbaya, hata hayo magari yangekuja hayawezi kusaidia, tunamwomba gavana Lusaka, atujengee hata barabara, sisi wenyewe tunaweza kujisaidia.” alisema mkazi huyo.

Chanzo cha mkasa huo hakijabainika huku maafisa wa usalama wakuendeza uchunguzi.