Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kimeondolewa katika uchaguzi unaotarajiwa baadaye mwaka huu, mmoja wa afisa wa tume ya uchaguzi amesema.

Hii ni baada ya kiongozi wa chama hicho Tundu Lissu kushtakiwa kwa madai ya kutaka kuvuruga uchaguzi.

Ramadhani Kailima, mkurugenzi wa uchaguzi katika Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi, alisema CHADEMA imeshindwa kutia saini hati ya kanuni za maadili zinazotarajiwa na hivyo kubatilisha ushiriki wake katika uchaguzi wa urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

“Chama chochote ambacho hakikutia saini kanuni za maadili hakitashiriki katika uchaguzi mkuu,” alisema, akiongeza kuwa marufuku hiyo pia itahusu chaguzi zote ndogo hadi 2030.

Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu, mgombea urais wa zamani, alishtakiwa kwa uhaini(charged with treason) siku ya Alhamisi.

Wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya upinzani wameishtumu serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa kisiasa, wakitaja msururu wa utekaji nyara na mauaji yasiyoelezeka. Serikali imekanusha madai hayo na imefungua uchunguzi juu ya utekaji nyara ulioripotiwa.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema hapo awali kwamba serikali inaheshimu haki za binadamu na imekanusha kuhusika katika ukiukaji wa haki za binadamu. CHADEMA haijatoa maoni juu ya uamuzi huu wa tume ya uchaguzi.

Mapema Jumamosi, chama hicho kilisema hakitashiriki katika sherehe ya kutia saini kanuni za maadili za uchaguzi, kama sehemu ya msukumo unaofanya kwa mageuzi.

Waendesha mashtaka walimshutumu Lissu siku ya Alhamisi kwa kutoa wito kwa umma kuanzisha uasi na kuzuia uchaguzi kufanyika. Hakuruhusiwa kuwasilisha ombi kwa shtaka la uhaini, ambalo lina adhabu ya kifo. CHADEMA hapo awali ilikuwa imetishia kususia uchaguzi isipokuwa mageuzi makubwa yatafanywa kwa mchakato wa uchaguzi ambao inasema unapendelea chama tawala.