Mbunge wa Kapseret Oscar Kipchumba Sudi ametoa shilingi milioni mbili kufanikisha ujenzi wa Kanisa moja la PCEA iliyoko katika Kaunti ya Kiambu, eneo la Githunguri.
Akizungumza na washirika wa Kanisa hilo la PCEA Githaithi leo Jumapili tarehe 13 Aprili, 2025, Sudi amenakili kuwa kumbukumbu yake anataka iwe ya kujenga makanisa.
Kulingana naye, yeye ni mkristo na siku atayoiaga dunia, ni tamanio lake watu wabaki wakimtaja kama “mtu ambaye alikuwa anapenda kujenga kanisa.”
Ameelezea kuwa aliweka kikomo kushiriki Harambee mwaka huu ila ya leo ilibidi ahudhurie kwani aliahidi rafiki yake Anne ambaye ni mshiriki wa Kanisa hilo.
“Mimi ni mkristo na desturi ya Kanisa ni kuja kuomba, kuombewa na unatoka ukiwa umefurahi. Niko hapa leo…Nilisema sitafanya Harambee mwaka huu nitafanya mwaka ujao lakini rafiki yangu Anne amenikumbusha nilikuwa nimemuahidi…Nimeona ile msingi mmeweka, ni msingi mzuri sana…Kule kwetu najenga kanisa nane. Siku yangu ya mwisho nataka waseme alikuwa anapenda kujenga kanisa. Hii kanisa isipoisha mtuite tena turudi. Kuna choir ya wazee nataka niwapimie uniform.”
Kando na hizo shilingi milioni mbili, Sudi pia ametoa shilingi elfu mia mbili (Ksh 200,000) kushonea waimbaji (choir) wa kanisa hilo sare.
Wenzake pia hawakuwachwa nyuma katika hafla hiyo ya matoleo. Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah ametoa Ksh 200,000, Sabina Chege Ksh 50,000, Mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek Ksh 100,000, William Kabogo Ksh100,000, Kiongozi wa Wanawake Kiambu Anne Wamuratha Ksh 100,000, rafikiye Sudi aliyetambulisha kwa jina Omondi ametoa Ksh 500,000 na wengineo.