Muungano wa Hospitali za Kibinafsi, (RUPHA), umeikosoa hatua ya wizara ya afya, kufunga na kushusha hadhi baadhi ya vituo vya afya, kwa madai kuwa vinaendesha shughuli zao bila leseni, usajili unaostahili, au kutoafikia viwango vinavyohitajika kutoka huduma za afya.
Kupitia mwenyekiti wao, Daktari Brian Lishenga, RUPHA imeelezea kuwa hatua hiyo haifuati utaratibu unaostahili, kama vile kufanyika kwa ukaguzi. Badala yake, wizara imelaumiwa kwa kufuta data muhimu kuhusu vituo vilivyoathirika kwenye mfumo, hali ambayo inadhoofisha utoaji wa huduma kutumia SHA.
”Wizara inafanya kinyume na utaratibu. Haiwezekani kujua idadi ya vitanda katika hospitali fulani bila ya kufanya ukaguzi.
Isitoshe, kuna sera inayoagiza wizara ya afya kutoa mwelekeo na muda maalum wa kuchukua hatua za marekebisho, iwapo itabaini hospitali imekiuka sheria au kudanganya kuhusu idadi ya vitanda vya wagonjwa ilivyo navyo.
Kama RUPHA, hatutetei hospitali zilizokiuka sheria. Tunaomba tu kwamba mchakato huo uzingatie taratibu na uzuiwe kuleta madhara kwa vituo vingine visivyo na hatia.” amesema Daktari.
Akizungumza jijini Mombasa wakati wa kikao na kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya, Waziri wa Afya Aden Duale ameibua tetesi kwamba baadhi ya hospitali hizo zinaendesha ulaghai, kwa kupokea wagonjwa wengi kuliko idadi wanayopaswa kuchukua, na kisha baadae kudai malipo zaidi ya SHA.
”Wagonjwa wengine wanalazimika kulala sakafuni huku wengine wakilala kitanda kimoja” Duale alisikitika
Ametoa onyo, na kuahidi kwamba msako huo utaendelea.
“Ni heri tuwe na hospitali mia moja pekee ambazo zinazingatia utu na usalama wa wagonjwa, kuliko hospitali elfu moja zinazolenga tu kupata faida.
Ikiwa unakusanya pesa na unataka wagonjwa zaidi, ni jukumu lako kujenga wodi ya ziada na kununua vitanda zaidi.”

Kufikia sasa, jumla ya hospitali 983 zimefungwa, na nyingine 487 kushushwa hadhi.
Written by Paul Muniu