Serikali ya Kaunti ya Kisumu imetangaza mpango wa kuwahamisha kwa muda wafanyabiashara wa Soko la Kibuye, ili kutoa nafasi kwa Serikali ya Kitaifa kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa soko hilo.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Mjini Kisumu Jumanne, Julai, Meneja wa Jiji Abala Wanga alisema shughuli hiyo itaanza rasmi mwezi Agosti, ambapo wafanyabiashara watahamishiwa Uhuru Business Park ili kuruhusu ujenzi kuendelea bila usumbufu.

“Tunawasihi wafanyabiashara wetu wakumbatie mradi huu kwa amani, ili tuharakishe uboreshaji wa Soko la Kibuye,” Wanga alieleza.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, baada ya kusimamiwa rasmi na Idara ya Makazi na Maendeleo ya Miji ya Serikali ya Kitaifa.

Hatua hiyo inafuata mazungumzo baina ya Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o na Rais William Ruto, ambapo Soko la Kibuye lilibainishwa kuwa mradi wa unaohitaji msaada ya kitaifa hivyo kufanywa kipaumbele.

Soko hilo linatarajiwa kukamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Ili kuepuka vikwazo, Wanga alieleza kuwa mazungumzo na wafanyabiashara yanaendelea ili kuhakikisha uhamisho unafanyika kwa utulivu na bila changamoto za kisheria.

“Tunazungumza na wafanyabiashara mara kwa mara kuhakikisha mchakato unakuwa laini na kuepuka ucheleweshaji,” aliongeza

Uboreshaji wa Soko la Kibuye unaendana na maono ya Gavana Nyong’o ya kuimarisha miundombinu ya masoko katika mji wa Kisumu. Tayari masoko ya Otonglo na Pap Onditi yamejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Kaunti.

Katika hatua nyingine, kaunti imeanza tathmini ya taa za barabarani ili kuboresha usalama. Wanga ameahidi kuchunguza mwenyewe taa zisizofanya kazi katika maeneo ya Nyalenda, Manyatta, Migosi na barabara kuu.

“Taa zinazofanya kazi husaidia kuongeza imani ya wafanyabiashara na kuimarisha shughuli za kiuchumi hata wakati wa usiku,” alisema.

Uboreshaji wa Soko la Kibuye ni hatua muhimu katika mchakato wa kuifufua Kisumu kama jiji la kisasa, akiwaahidi wafanyabiashara kituo cha kisasa na kuongeza uwezo wa uchumi wa jiji.