Ofisi ya Rais itawaandalia washindi wa Tamasha la Kitaifa la Drama na Filamu hafla maalum ya tamasha la kitaifa (State Concert) itakayofanyika Jumatano, Aprili 16, 2025, katika Ikulu ya Nakuru.

Tamasha hiyo itahusisha maonesho kutoka kwa shule bora zilizofanya vyema kwenye Tamasha la Kitaifa la Drama na Filamu la Shule za Kenya la mwaka huu, wa 2025.

Miongoni mwa shule zilizong’aa ni Moi High School Mbiruri kutoka Kaunti ya Embu, Kanyuambora High School, na Kangaru High School, ambazo zote zilitambuliwa kitaifa kwa ubunifu wao wa hali ya juu.

Tamasha ya mwaka huu ilivutia hisia kubwa za umma, hasa kutokana na mjadala uliozuka kufuatia tamthilia ya Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere ‘’Echoes of War.’’

Tamthilia hiyo, iliyochambua masuala ya kisiasa, ilisababisha mjadala mpana kitaifa na kuvutia maoni tofauti kutoka kwa washikadau wa elimu na umma kwa jumla.

Kulingana na mwaliko kwa vyombo vya habari uliotolewa na, Katibu wa Mawasiliano wa Ikulu, Emmanuel Talam vyombo hivyo, vinatakiwa kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya kuidhinishwa kabla ya kuingia kwenye eneo la hafla.

Tamasha hili ni kilele cha Tamasha ya Kitaifa la Drama na Filamu, ambayo huadhimishwa kila mwaka kama jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa shule na vyuo kote nchini.

Kwa miongo kadhaa sasa, tamasha hii imekuwa likionesha vipaji mbalimbali katika sanaa za maigizo, ngoma za kitamaduni, filamu, na simulizi za kisasa kupitia njia za kidijitali.

Tamasha hii ya Ikulu hutoa fursa kwa shule na vikundi  vilivyotia fora kuonesha vipaji vyao mbele ya viongozi wakuu wa serikali, wageni mashuhuri, walimu, na Rais mwenyewe.

Aidha, tamasha hii hutambuliwa kama jukwaa la kitaifa la kuangazia mchango wa sanaa katika elimu, uhamasishaji wa kijamii, na kuhifadhi tamaduni.

Makala ya mwaka huu yanafanyika mjini Nakuru, hatua inayodhihirisha juhudi za serikali za kusambaza hafla za kitaifa na kuimarisha ushirikishwaji wa maeneo mbalimbali.