Kaunti ya Mombasa imezindua ujenzi wa hifadhi ya kisasa ya maiti katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Coast General, kwa nia ya kupunguza msongamano wa miili.
Mradi huo unaofadhiliwa na mfadhili wa binafsi, utaongeza uwezo wa hospitali hiyo kuhifadhi mili 90 kwa wakati mmoja, hivyo kufikisha idadi ya mili inayoweza kuhifadhiwa katika chumba hicho kufikia 325.
Mkurugenzi Mkuu wa Coast general, Daktari Iqbal Khandwalla, ameItaja hatua hiyo kama kigezo muhimu katika kupandishwa ngazi kwa hospitali hiyo.
“Ujenzi wa chumba kipya cha kuhifadhia maiti utakapokamilika, kutakuwa hakuna msongamano tena wa maiti wala harufu iliyokuwa ikihanikiza. Chumba kipya kitapandisha hadhi ya hospitali hii,” Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, amesema.
”Ujenzi wa makafani ya kisasa si tu uboreshaji wa muundo. Ni kauli ya utu, na inaakisi dhamira ya serikali yetu ya kuheshimu uhai hata katika hatua yake ya mwisho”
Spika wa Bunge ya Kaunti ya Mombasa Aharub Khatri, vilevile amejitolea kufadhili sehemu maalum, ya kuandaa mili ya waislamu katika hospitali hiyo, kabla ya mazishi.
Mbali na hayo, serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia Gavana Abdulswamad Shariff Nassir, imetangaza juhudi za kuimarisha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Coast General, ili itambulike na kupandishwa ngazi ya sita, kutokana na miundombinu na huduma zake.

Gavana huyo, ameelezea kuwekezwa katika vituo kadhaa za matibabu maalum, kama vile kituo cha saratani, kile cha dharura, cha hali mahututi na hata ujenzi wa chumba kipya cha kuhifadhia maiti, juhudi ambazo ametaka zitambulike na wizara ya afya.
Changamoto kuu katika hospitali hiyo ikiwa ni msongamano wa wagonjwa, serikali ya Mombasa imeazimia kuimarisha hospitali nyingine za umma, ili kupunguza idadi ya rufaa katika Hospitali ya Rufaa ya Coast General.
Coast General, ni Hospitali Kuu ya Level 5 katika Ukanda wa Pwani, inayowahudumia wakaazi kutoka kaunti mbali mbali, ukanda huo.
Written by Paul Miniu