Polisi mjini Nyahururu Alhamisi wamemkamata mshukiwa mmoja na kupata simu za rununu zinazoaminika kuwa za wizi.

Simu 50, tableti tatu na kompyuta vilipatikana kwenye kibanda kilichoko katika kituo cha mabasi cha Nyahururu mjini.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Nyahururu, Bernard Odino, alisema inaaminika kuwa mshukiwa ni mwanachama wa kundi la wezi wa simu linaodaiwa kuwa na uhusiano hadi nchi jirani.

“The stolen phones are transported to Uganda where we believe the network has found a market,” the alisema afisa huyo

Alisema kumekuwa kukishuhudiwa ongezeko la visa vya wizi mitaani katika siku za hivi karibuni katika miji ya Nyahururu na miji mikubwa katika Kaunti ya Laikipia ambapo watu huibiwa pesa na simu.

Odino alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuondoa vibanda na miundo msingi isiyopangwa karibu na kituo cha mabasi cha Nyahururu akisema ni maficho ya wahalifu na wanyang’anyi.

Odino alikuwa akizungumza katika kituo cha polisi ambapo mali hiyo ilioneshwa kwa wanahabari, akiwa ameandamana na Mkuu wa Kituo (OCS) Isaac Kimutus.

Kupatikana kwa simu hizo kumejiri siku mbili tu baada ya polisi kupata vifaa vya kielektroniki na bidhaa nyingine za nyumbani na kuwakamata washukiwa wawili, wakiwamo mvulana mwenye umri wa miaka 24.

Bidhaa hizo zenye thamani ya takriban Shilingi 600,000 zilipatikana wakati wa msako wa usiku katika nyumba ya kupanga karibu na kiwanda cha New KCC mjini Nyahururu.

Washukiwa hao wawili wanaodaiwa kuwa ni ndugu walikamatwa wakati wa msako huo Jumatatu usiku.

Mali iliyopatikana ni pamoja na runinga saba, simu 12 za rununu, vitambulisho vitano vya taifa, baiskeli mbili na pikipiki moja, miongoni mwa vitu vingine vyote vikiwa na thamani ya takriban Sh600,000.