Hali ya sintofahamu na vurugu imeshuhudiwa katika eneo la Railways Stage, Bondeni, katika Kaunti ya Nakuru, baada ya wakazi na vijana wa eneo hilo kukabiliana na maafisa wa serikali wakipinga mpango wa kusimamia upya vibanda na maeneo ya biashara bila kushirikishwa.

Wakiongozwa na Miriam Ngema, wakazi hao wamelalamikia ukosefu wa uwazi, wakisema hakuna mwakilishi rasmi wa Bondeni, hivyo maamuzi yanapaswa kufanywa kwa ushirikiano na jamii nzima.

“Sisi hatuna shida na serikali ya kaunti. Lakini tuna shida, hii mikutano inayofanyika usiku. Jamii imefanya kazi hapo, wanachosubiri sasa ni vibanda. Tumevumilia, mikutano imekuwa ikifanyika usiku tukiwa kimya, lakini wakati huu hatutanyamaza,” alisema Miriam


Mustafa Ndegwa, mmoja wa viongozi wa vijana, amesema vijana walioacha uhalifu, wanahitaji nafasi katika miradi hiyo na pia ajira.

Kufuatia hali hiyo, Waziri wa Biashara, Utalii na Utamaduni katika Kaunti ya Nakuru, Kuria Muiruri, ametoa hakikisho kwa wakazi hao, akisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote aliyegawiwa nafasi katika soko la Ziwani kwa sasa. Akizungumza na wanahabari, Muiruri amesema serikali imeanza mashauriano na washikadau katika sekta ya Matatu na biashara ili kuweka mpango wa pamoja.


“Stage yetu haijaisha, lakini ikikamilika kila mshikadau atashirikishwa,” alisema Kuria, ‘leo ilikuwa siku ya wadau wa matatu na siku zingine zitatengwa kwa wafanyabiashara wa sekta zingine kama mama wa vibanda, vijana wa car wash na wauzaji wa chakula.’’


Waziri huyo amekemea vikali viongozi wanaochochea wakazi kupinga mpango huo, akisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa maendeleo. “Tunahitaji amani, bila hivyo, hakuna biashara wala wateja watakaofika pale,” alisema.


Ameahidi kuwa serikali itaendelea kusikiliza maoni ya kila kundi na hakuna mfanyabiashara atafurushwa kiholela, bali nafasi zitapanuliwa kwa utaratibu na haki kwa wote.

Written by, Allan Wetungu