Kwa saa kadhaa, Alhamisi asubuhi, maelfu ya watu walishindwa kuvuka kutoka au kuelekea kisiwani Mombasa, hali ambayo ilileta kizaazaa kwani watu walig’ang’ania kuingia kwenye feri, hivyo kuhatarisha maisha yao.

Huduma ya ferry nchini ilitoa taarifa kudhibitisha kwamba feri mbili: MV. Kwale na Harambee, zilikuwa zikihudumu wakati huo, licha ya kwamba kivuko hicho kina feri sita ambazo zinapaswa kuhudumu.

Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa watu na magari, ikisambaratisha shughuli zao za kuelekea kazini.

Waliojipata katika msongamano huo wamelalamikia huduma duni za feri, ambazo kwa sasa zinasimamiwa na Halmashauri ya Bandari ya Mombasa, KPA. Akizungumza na Radio 47, Richard, makaazi wa Likoni alilalamika;

“Feri zinazohudumu ni mbili, lakini feri zilizoegeshwa katika kivukio hiki ni takriban feri saba. Hali hii inasababisha msongamano mara kwa mara, ilhani ni njia muhimu kwa watalii ambao wanaenda sehemu za Diani na ukunda, wakaazi wa Likoni na hata wale wanaosafiri kuelekea mpaka wa Kenya na Tanzania.”

Mkazi mwingine, Cornelius Onkopa ameulaumu usimamizi wa huduma ya feri na Mamlaka ya Bandari ya Mombasa KPA, kufuatia changamoto za msongamano.

“Ikiwa feri inachangamoto na inapaswa kukarabatiwa, ni vyema wakaazi wajulishwe, ili waweze kujipanga. Hali ya leo imefanya wengi kuchelewa kazini. Wengine wetu hatukwenda kazini…tulituma udhuru. Isitoshe, kunao ambao wameumia kutokana na msongamano huo.”

Ukiwa ni msimu wa Pasaka, idadi kubwa ya watu na watalii hupendelea kutumia kivuko cha Likoni kuelekea maeneo ya watalii, Diani, Kaunti ya Kwale, hali inayochangia kuongezeka kwa abiria wa feri, hususan wakati wa asubuhi na jioni.

Mnamo tarehe 5 mwezi Februari mwaka huu, kulishuhuduwa tukio jingine la msongamano katika kivuko cha Likoni, ambapo abiria waliwarushia mawe walinzi wa huduma za feri, kwa kukosa uvumilivu wakati wa kusuburi feri zilizokuwa zikihudumu, huku walinzi nao wakijibu kwa kuwarushia mawe abiria.

Mamlaka ya huduma za ferry kaunti ya Mombasa ilitoa taarifa ikikashifu vurugu zilizotokea na kuwaelekezea lawama walinzi wa usalama wa Ismax, waliopewa jukumu katika kivukio cha Likoni, wakidai kuwa hatua zilizochukuliwa na walinzi hao hazikustahili, hivyo kukiuka maadili msingi ya mamlaka ya bandari ya Mombasa.

Meneja wa huduma za usalama kivuko cha Likoni Tony Kibwana, aliagiza kampuni ya usalama ya Ismax kuandika majibu kuhusu tukio hilo ndani ya saa 24, ili Mamlaka ichukue hatua zinazostahili kuhusu suala hilo.

Usimamizi wa feri aidha ilirejesha huduma ya feri ya tatu, na kurejesha hali ya kawaida katika kivukio cha Likoni.

Written by, Paul Muniu