Aliyekuwa Waziri wa Usalama Dakta, Fred Matiang’i, amerejea nchini kutoka Marekani, huku kukiwa na tetesi kuhusu nia yake ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Matiang’i aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA kutumia ndege ya Qatar Airways akitokea Washington kupitia Qatar.
Hata hivyo, alikataa kuzungumza na wanahabari lakini “alimshukuru Mungu kwa safari njema” bila kurekodiwa rasmi, akisema atalihutubia taifa baadaye.
Alipokelewa na viongozi kadhaa akiwamo Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo, na Seneta Maalum wa UDA Gloria Orwoba.


Kurejea kwa Matiang’i kunajiri baada ya Chama cha Jubilee kudokeza kuwa kitampendekeza kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza Januari 25 wakati wa kikao na viongozi wa Jubilee katika Kaunti ya Narok, Kioni alitangaza kuwa chama hicho kinachoongozwa na Uhuru Kenyatta kimemchagua Matiang’i kumkabili Rais Ruto katika uchaguzi huo.
Kioni alisema hivi, “Fred Matiang’i is the one they are saying is in Jubilee. He worked with the party for 10 years. So, we, as the Jubilee party, have our own candidate, Fred Matiang’i. He will face off with other candidates to ensure President William Ruto goes home. You have to start registrations and send the message to the people, and we don’t want fights.”
Matiang’i mwenyewe hajazungumzia suala la kujitosa katika kinyang’anyiro mwaka 2027 ila kumekuwa na shinikizo za kumtaka awanie urais. Hata hivyo, mjadala ungali unaendelea kuhusu nani anatosha baina ya Matiang’i na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kumbabili Ruto.
Tayari Maraga ametangaza kuwa yu tayari kujitosa debeni mwaka 2027. Sasa swali ni je, nani kati ya Matiang’i na Maraga ambao wote ni wazaliwa wa Kaunti ya Nyamira atakayepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi pamoja na wananchi?