Maafisa wa Idara ya Upelelezi DCI wamemkamata Samuel King’ara Kimani, mshukiwa mkuu wa mauaji ya kikatili ya wanawake wawili katika Kaunti ya Kiambu.
Kufuatia juhudi za pamoja, wapelelezi wa kitengo cah kukabilia mauaji walimkamata mshukiwa mkuu kutoka mafichoni katika eneo la Ngomongo, Nairobi, tarehe 14 Aprili, 2025.
Kimani anahusishwa na mauaji ya Rosemary Njeri Ndekei mwenye umri wa miaka 22, na Hellen Wambui Ndung’u mwenye umri wa miaka 20, mauaji yaliyozua mshtuko mkubwa si tu kwa wakazi wa Kaunti ya Kiambu bali pia kwa taifa kwa ujumla.
Mauaji ya Ndekei Katika kisa cha kwanza, Ndekei alitoweka tarehe 17 Machi, 2025 alipokuwa akielekea mjini Thika kununua mavazi.
Kutoweka kwake kulisababisha wasiwasi, na taarifa ya kutoweka ilitolewa katika Kituo cha Polisi cha Thika na mpenzi wake na ndugu zake. Kwa bahati mbaya, mwili wake uligunduliwa na wananchi katika shamba la kahawa katika eneo la Karibaribi tarehe 18 Machi, 2025.
Mwili wa Ndekei, ambao ulikuwa umeoza, ulisafirishwa hadi katika Hifadhi ya Maiti ya General Kago kwa uchunguzi na utambuzi. Tarehe 19 Machi, 2025, mwili ulitambuliwa na familia yake.
Uchunguzi wa mwili ulionesha kwamba alifariki dunia baada ya kunyongwa kwa nguvu na majeraha ya kichwa, dalili za mauaji ya kikatili.
Mauaji ya Ndung’u katika kisa cha pili; Ndung’u alitoweka tarehe 31 Machi, 2025 alipokuwa amemtumwa na mama yake kununua vyakula katika Kituo cha Biashara cha Ngorongo, Gatundu Kaskazini.
Kesho yake, mwili wake ulipatikana katika kichaka, ukiwa umefunikwa kidogo na mchanga. Mwili huo haukuwa na majeraha ya wazi, na majirani walimtambua kama msichana aliyekuwa ametoweka.
Kundi la wapelelezi lilifuatilia na kumkamata mshukiwa mkuu katika eneo la Dry, Ngomongo tarehe 14 Aprili, 2025.
Uchunguzi wa awali umeonesha mtindo wa kijasusi wa kutisha: katika visa vyote, mshukiwa alikutana na wasichana anaoaminika kuwaua kwenye njia zisizo na watu, kisha kuwavuta hadi kwenye mashamba makubwa ya kahawa, ambapo aliwadhulumu kisha kuwaua kikatili.
King’ara alifikishwa mahakamani tarehe 16 Aprili, 2025, ambapo mahakama ilikubali ombi la kuendelea kumzuilia hadi uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.