Wakristo duniani kote waadhimisha Ijumaa Kuu; kumbukumbu ya kuteswa, kusulubiwa na kufa kwa Yesu Kristo msalabani.
Kulingana na imani ya Wakristo Ijumaa Kuu, ni siku takatifu isiyo ya kawaida. Kwa mfano, kulingana na Imani ya Kikatoliki Ijumaa Kuu misa haifanyiki, bali waumini hukusanyika kwa Ibada, kusoma injili kuhusu mateso na kufanya njia ya msalaba.
Kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ya Pasaka, Kanisa linaingia katika kilele cha Misa ya Pasaka ambapo:
Ijumaa Kuu inakuwa ni tafakari ya Msalaba, Jumamosi Kuu inakuwa kimya, waumini wakisubiri matumaini na usiku, huadhimishwa Mkesha wa Pasaka yaani ibada takatifu yenye ishara za mwanga, maji, injili na sakramenti.
Kisha Jumapili ya Pasaka, hufanyika sherehe ya Ufufuko wa Kristo kuashiria ushindi dhidi ya dhambi na mauti.
Hatimaye Jumatatu ya Pasaka huwa ni siku ya kuendeleza furaha ya kiimani kwamba Yesu Kristo yu hai baada ya kushinda mauti.
Katika siku hizi takatifu, wakiristo huhimizwa kushiriki kwa moyo wote, kwa njia ya sala, tafakari, na sakramenti, hasa upatanisho na Ekaristi.
Ikumbukwe Alhamisi kabla ya Ijumaa Kuu inayojulikana na wakristo kama Alhamisi Kuu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, aliletembelea gereza la Regina Coeli la mji Roma ikiwa ni sehemu ya desturi ya miaka mingi kukumbuka siku ambayo Yesu Kristo aliwaandalia karamu ya mwisho na kuwaosha miguu wafuasi wake 12 kabla ya kusulubiwa.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Injili ya Wakisto, Yesu alifufuka siku tatu baada ya kuteswa na kufa msalabani na siku hiyo husherehekewa kama sikukuu ya Pasaka.