Shirika la Anga za Juu la Kenya (Kenya Space Agency) KSA limetoa taarifa rasmi ya tahadhari kwa umma kuhusu uwezekano wa kuanguka kwa kifaa cha angani (space debris), kikubwa ambacho huenda kikapitia anga ya Kenya kati ya tarehe 19 na 20 Aprili 2025.

Kifaa hicho, chenye nambari ya utambulisho Norad ID 61909/2024-205R, ni mabaki makubwa ya roketi yenye uzito ambao bado haujafahamika. Kulingana na ramani ya mwelekeo wa safari yake, mabaki hayo yanatarajiwa kupita katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwamo Kenya kutoka Kaskazini Mashariki kuelekea Kusini Mashariki kuelekea Tanzania na kwingineko kusini.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mabaki hayo yanatarajiwa kuingia tena katika anga ya dunia siku ya Jumamosi, tarehe 19 Aprili 2025, saa 5:15 usiku, kwa makadirio ya muda yaliyo na tofauti ya hadi saa 15 na dakika 46. Hii ina maana kuwa yanaweza kuanguka wakati wowote kati ya saa 1:29 asubuhi Jumamosi hadi saa 9:01 alasiri Jumapili, 20 Aprili 2025.

Wakenya wameonywa kuwa kifaa hicho kinaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali sehemu kitakapopitia kutokana na ukubwa wake. Ingawa mabaki haya hayatarajiwi kuanguka moja kwa moja nchini Kenya, tahadhari imetolewa kwa wananchi kuwa makini.

KSA imesema inaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa kufuatilia na kutoa utabiri sahihi zaidi wa njia na muda wa kuingia tena kwa mabaki hayo katika anga ya dunia. Ramani ya mwelekeo wa ardhi (Figure 1) imetolewa kuonesha njia inayotarajiwa kufuatwa na kifaa hicho.

Wananchi wamehimizwa kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa haraka kwa vyombo vya usalama, ikiwa wataona kitu chochote kisicho cha kawaida kikidondoka au kuruka angani ndani ya kipindi hicho. Taarifa zinaweza kutolewa kupitia kituo cha polisi kilicho karibu, ofisi ya utawala wa serikali au kambi ya jeshi.

Kwa sasa, Wakenya wanashauriwa kuwa waangalifu bila kuingiwa na hofu huku wataalamu wakiendelea kufuatilia hali hii kwa karibu.