Kikosi Maalum cha Operesheni Jijini Nairobi kimefanya msako mkali dhidi ya ulanguzi wa mihadarati, ambapo maeneo matatu yanayohusishwa na biashara hiyoharamu yamelengwa.
Katika taarifa ya polisi maafisa wamefanikiwa kunasa mihadarati kwa wingi. Maeneo ambapo msako huo umefanyika ni Huruma, Karen na katikati mwa jiji, barabara ya Kirinyaga
Katika msako huo, polisi wamenasa kilo 160 za bangi, misokoto 2,353 ya bangi iliyokunjwa tayari kwa matumizi, maganda na karatasi maalum za kufungia bangi pamoja na “filter tips”
Mashine mbili za kupima uzani na pikipiki mbili zinazoaminika kutumika kusafirisha dawa hizo za kulevya.
Washukiwa watano wametiwa mbaroni wakati wa operesheni na wanaendelea kuzuiliwa na polisi huku wakisubiri kufikishwa mahakamani. Washukiwa hao ni Duncan Irungu, Dakiwako Wako, Geoffrey Omenya Lukwede, Joseph Maina,George Odhiambo Owuor.
Maafisa wa usalama wamethibitisha kuwa oparesheni bado inaendelea huku wakitoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na biashara haramu ya ulanguzi wa mihadarati.