Watu wasiopungua 143 wamefariki dunia na wengine kadhaa hawajulikani waliko baada ya boti iliyobeba mafuta kushika moto na kuzama katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo DRC, maafisa walisema Ijumaa.
Mamia ya abiria walikuwa wamejazana kwenye boti ya mbao kwenye Mto Kongo Kaskazini-Magharibi mwa DRC Jumanne wakati moto ulipozuka.
Kisa hicho kilitokea karibu na Mbandaka, mji mkuu wa Jimbo la Equateur, katika makutano ya mito ya Ruki na Kongo; mto wa kina zaidi duniani.
Video ambazo zimeenea mitandaoni zinaonesha moto ukitoka kwenye boti ndefu iliyokwama mbali na ufuo, moshi ukitoka kwenye mabaki huku watu walioko kwenye boti ndogo wakitazama kwa hofu.
Idadi kamili ya abiria waliokuwa kwenye boti hiyo haijajulikana.
Baadhi ya walionusurika waliokolewa na kulazwa hospitalini. Lakini kufikia Ijumaa, familia kadhaa bado hazina taarifa kuwahusu wapendwa wao.
Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati inakabiliwa na ukosefu barabara zinazopitika na ndege uhudumu katika maeneo machache tu.
Kutokana na hali hiyo, watu mara nyingi husafiri kwa kutumia maziwa, Mto Kongo ambao ni wa pili kwa urefu Barani Afrika baada ya Nile na vijito vyake vyenye miinuko mingi, ambako ajali za boti na mashua ni za mara kwa mara na huwa na idadi kubwa ya vifo.
Ukosefu sugu wa orodha za abiria mara nyingi huchangia ugumu katika shughuli za uokoaji.
Oktoba 2023, watu wasiopungua 47 walifariki dunia baada ya boti kuzama kwenye Mto Kongo katika jimbo la Equateur.
Zaidi ya watu 20 walifariki Oktoba mwaka jana boti ilipozama katika Ziwa Kivu mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo.
Ajali nyingine ya boti kwenye Ziwa Kivu ilisababisha vifo vya karibu watu 100 mwaka 2019.