Watu wanne wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya iliyotokea mapema Ijumaa katika Barabara ya Northern Bypass karibu na Daraja la Membley, Kaunti ya Kiambu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kituo cha trafiki cha Ruiru, ajali hiyo iliripotiwa saa 04:45 asubuhi na ilitokea majira ya saa 03:42. Ajali hiyo ilitokea baada ya gar ndogo kugonga trela upande wa nyuma, huku dereva na abiria watatu wakifariki.

Ripoti ya awali ilieleza kuwa trela hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Kahawa West kuelekea mzunguko wa barabara wa Membley, na wakati ilipofika eneo la tukio, gari hilo ndogo lililigonga kwa nguvu kutoka nyuma. Madhara ya ajali hiyo yalikuwa makubwa kiasi kwamba wote waliokuwa ndani ya gari dogo walifariki papo hapo.

Miili ya waliofariki imepelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Thika General, ikisubiri utambuzi rasmi na kufanyiwa upasuaji . Maafisa wa polisi wa trafiki walifika katika eneo la tukio na kulikagua kwa kufuata taratibu zote za uchunguzi.

Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali.