Wakristo kote duniani wanaadhimisha Jumapili ya Pasaka; moja ya Siku Kuu muhimu zaidi, ambapo Wakristo hasa wa kanisa Katoliki, Anglikana, Lutheran na Orthodox wanasherehekea ufufuko wa Yesu Kristo. Tukio hili ni msingi wa imani ya Wakristo, kwani Yesu alishinda kifo na dhambi, na kwa kumfuata, wanaamini ahadi ya uzima wa milele. Pasaka ni ishara ya ushindi wa Kristo dhidi ya mauti, na ni kipindi cha furaha na upya wa kiroho.
Kabla ya Jumapili ya Pasaka, kuna Jumamosi Kuu, siku ya kimya na tafakari. Hii ni siku ambapo Wakristo wanakumbuka kifo cha Yesu msalabani na huzuni ya kumkosa. Ni siku ya maombolezo, lakini pia ni siku ya kujiandaa kwa furaha ya ufufuo.
Katika imani ya Kikatoliki, Jumamosi Kuu hakuna Misa hadi jioni, ambapo Misa ya Pasaka inaanza. Mshumaa wa Pasaka unawashwa kama ishara ya nuru ya Kristo inayoangaza giza la kifo.


Katika sherehe ya Misa ya Pasaka, Wakristo wanakumbuka na kusherehekea ufufuo wa Yesu Kristo, ambaye alitimiza mpango wa Mungu wa wokovu.
Ufufuo wake unadhihirisha nguvu ya Mungu na upendo wake kwa wanadamu. Pasaka inawakumbusha Wkiristo kuwa, kupitia imani katika Kristo, wanapata msamaha wa dhambi na ahadi ya uzima wa milele.