Hospitali ya Mediheal ambayo imehusishwa na upandikizaji wa Figo kwa njia isiyo halali imepinga madai hayo.
Swarup Mishra ambaye ni Mwanzilishi wa Hospitali hiyo amevunja kimya chake na kuitetea hospitali hiyo akisema i katika viwango vya kimataifa kwani imefanya upandikizaji kwa raia wa mataifa mbalimbali ikiwamo Israeli, Somalia, Uganda miongoni mwa mengine hivyo madai dhidi yao si ya kweli.
Kadhalika Mishra amesema kuwa wagonjwa 476 kutoka humu nchini na mataifa ya nje wamefanyiwa upandikizaji kufikia sasa tangu hospitali hiyo ilipopata idhini ya kutoa huduma hiyo mwaka wa 2018.
Mishra amesema japo miongoni mwa wagonjwa hao kumi wamefariki dunia kutokana na sababu mbalimbali na hakuna aliyepata ubandikizaji wa figo ambaye ameaga dunia.
Hospitali hiyo aidha imesisitiza kuwa upandikizaji hauwezi kufanywa bila idhini ya wanaohusika hivyo madai kuwa ni hospitali yenyewe iliyokuwa ikiwatafutia wagonjwa figo si ya kweli.

Kando na hayo Mishra amesema kuwa huduma za matibabu katika hospitali hiyo ni bora zaidi jambo ambalo linachangia wagonjwa kutoka kwenye mataifa ya nje kupata matibabu hospitalini humo vilevile gharama ya chini.
Alisema, “Gharama ya matibabu kwenye hospitali hii ni dollar elfu 25 kwa wagonjwa wa humu nchini na dollars elfu 35 kwa wagonjwa kutoka mataifa ya nje”
Kuhusu hali yake kwa Sasa kutokana na madai hayo pamoja na kusimamishwa kazi kwa mda, Mishra amesema serikali ilichukua hatua sahihi kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi na kusema kuwa angechukua hatua hiyo mwenyewe lakini madai hayo yaliibuka akiwa nje ya nchi. Mishra amesema hana hatia yoyote na yuko tayari kuwajibishwa kisheria endapo atapatikana na hatia.
Written by, Charity Papai