Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limezindua ripoti kuhusu madhila wanayoyapitia Wakenya wanaofanya kazi za nyumbani nchini Saudia Arabia.
Ripoti hiyo imeelezea umuhimu wa kubuniwa kwa sera za kulinda haki za wafanyikazi hao, kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Uzinduzi wa ripoti hiyo umefanyika jijini Mombasa, na kuwaleta pamoja waathiriwa, watetezi wa haki na wataalamu mbalimbali.
Taifa la Saudia Arabia lina wafanyakazi takriban milioni nne wanaofanya kazi za nyumbani, wote wakiwa ni raia wa kigeni.
Hata hivyo, visa vingi vya masaibu ya baadhi ya wanawake kutoka Kenya walioajiriwa humo vimeripotiwa, wengi wakisimulia mazingira ya utumwa, kufanyishwa kazi bila mapumziko, kufungiwa ndani ya nyumba, kubaguliwa, na hata kudhulumiwa kingono.

Kidambi Omar, mkazi wa Tiwi kwenye kaunti ya Kwale, ni mmoja wa waathiriwa, akisimulia kwamba alikosa kushugulikiwa na mwajiri wake wakati akiwa mgonjwa.
“Mwajiri wangu alikuwa hanishugulikii nikiwa na tatizo la afya. Nikiwa mgonjwa ilikuwa ni shida sana, ilikuwa ikinilazimu kupiga simu katika ofisi za uhamiaji ili wanipeleke hospitali. Walikuwa wakinitisha kuwa wangekata mshahara wangu kipindi nikiwa hospitalini. Changamoto nyingine ni kwamba nilikuwa nikilala kuchelewa na kuamka mapema, na hivyo kukosa muda wa mapumziko.”
Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International Irungu Houghton, alifafanua ripoti hiyo, huku akisisitiza haja ya serikali ya Kenya kushirikiana na ile ya Saudi Arabia kukabili udhalimu huo.
“Ripoti hii imenakili simulizi za unyanyasaji wa kingono na ubakaji, huku pasipoti za waajiriwa zikichukuliwa ili wasiweze kukimbilia usalama. Kile ambacho tunasisitiza ndani ya ripoti hii ni kwamba ni lazima udhalimu huu ukomeshwe! Serikali ya Saudia Arabia sharti iwachukulie wakenya kama raia wao. Kuna mapendekezo pia kwa serikali ya Kenya, ambapo tumeihimiza kukabiliana na mawakala ambao hawajasajiliwa, kwani wanahusika pakubwa katika kuwalaghai wakenya wanaosafiri kutafuta kazi za nyumbani katika mataifa ya kigeni.”
Ripoti ya Amnesty International, inaitaka Saudi Arabia kuondoa kabisa mfumo wa Kafala, mfumo unaoruhusu waajiri kudhibiti wafanyikazi wao, na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa nyumbani wanapata haki na ulinzi sawa na wafanyakazi wengine wote.
Aidha, inaitaka serikali ya Kenya kupitisha mikataba muhimu ya kimataifa ya haki za binadamu, kuwajumuisha wafanyakazi wahamiaji chini ya masharti ya sheria ya kazi, na kupendekeza mshahara usiopungua kiwango fulani kwa wafanyakazi hao.
Written by, Paul Muniu |